Moja kwa moja, Zelensky apendekeza mazungumzo ya ana kwa ana na Putin ili kumaliza vita vya Ukraine

Kupitia barua ya wazi aliyomwandikia Putin, Zelensky alisema kuwa ni muhimu viongozi hao wawili kukutana moja kwa moja ili kujadili njia za kurejesha amani kati ya Urusi na Ukraine.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Utawala wa kijeshi Mali watoa zawadi nono kwa kiongozi wa kundi la al-Qaeda

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya kijeshi ya Mali inatoa dola milioni 3.5 kwa taarifa zitakazowezesha kukamatwa au kuuawa kwa Iyad Ag Ghaly. Serikali hiyo pia inatoa zawadi ndogo kwa washukiwa wengine, ikiwa ni pamoja na watu wanaotaka kujitenga kwa Tuareg.

    Kikosi tawala cha kijeshi nchini Mali kimetoa zawadi ya dola milioni 3.5 (kama euro milioni 3) kwa habari zitakazopelekea kukamatwa au kuuawa kwa Iyad Ag Ghaly, ambaye anaongoza tawi la Sahel la kundi la kigaidi la al-Qaeda lililoanzisha mashambulizi makubwa mnamo mwezi Aprili.

    Ghaly, chifu wa Jama'at Nusrat al-Islam wal-Muslimin (JNIM), anasakwa na nchi kadhaa za eneo la Sahel barani Afrika, ambazo kadhaa zinatawaliwa kijeshi.

    Mwezi Aprili, JNIM iliungana na waasi wa Tuareg kuanzisha mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya serikali ya Mali katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja. Mashambulio mengine ya wakati huo huo yaliua watu kadhaa, akiwemo Waziri wa Ulinzi Sadio Camara.

    JNIM ndilo kundi kubwa zaidi la Kiislamu linalopigana na wanajeshi katika eneo la Sahel, ambapo makundi mengi ya Kiislamu yenye itikadi kali na wanaotaka kujitenga yanaendesha shughuli zake.

    Soma zaidi:

  2. Sudan, DR Congo ziko kwenye migogoro mikubwa zaidi duniani iliyopuuzwa - NRC

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ziko kwenye orodha ya migogoro ya wakimbizi iliyopuuzwa zaidi duniani, kundi la misaada la Wakimbizi la Norway limesema.

    Sudan, ambayo tangu 2023 imekumbwa na mzozo wa umwagaji damu kati ya majenerali wawili wapinzani wanaoshindania madaraka, ina zaidi ya watu milioni tisa waliokimbia makazi yao, taarifa ya shirika hilo ilisema.

    Shirika hilo liliongeza kuwa Wasudan wengine milioni nne wamekimbilia nchi jirani na karibu watu milioni 19.5, pia wanakabiliwa na njaa.

    "Ni jambo lisiloweza kufikirika kwamba mgogoro wa wakimbizi wa kiwango sawa na migogoro ya Syria na Ukraine katika kilele chake unaweza kuendelea kuwa mbaya zaidi bila kutambuliwa," mkuu wa NRC Jan Egeland alisema.

    Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako miongo ya vita na mlipuko wa Ebola umefanya hali kuwa mbaya zaidi.

    "Watu husahau kwamba kutakuwa na magonjwa ya mlipuko, harakati za uhamiaji, na upotezaji mkubwa wa maisha ya binadamu ikiwa hatuwekezi katika matumaini katika mabara mengine", Egeland amesema.

    Alisema kuwa Afrika iko upande wa Mediterania, wanakoenda likizo na ikiwa bara hilo litaathirila, pia nao watakabiliwa na madhara yake.

    Soma zaidi:

  3. Ethiopia: TPLF yahimiza hatua za kimataifa kuzuia vita vinavyokaribia

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Chama cha TPLF nchini Ethiopia, kimeonya kuwa taifa hilo linakabiliwa na hatari ya kuzuka kwa mzozo mkubwa na wenye madhara makubwa, huku kikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kabla hali haijawa mbaya zaidi.

    TPLF imesema kupitia taarifa iliyotolewa jana Juni 4, wakati Ethiopia ikihitimisha uchaguzi wake mkuu wa 7, kuwa uchaguzi hauwezi kutatua mzozo wa kisiasa unaozidi kuongezeka nchini humo na kwamba changamoto za sasa za Ethiopia zinahitaji mazungumzo ya kitaifa yenye umoja na ya kuaminika yenye uwezo wa kushughulikia matatizo ya kimsingi ya kisiasa ya nchi hiyo.

    TPLF, ambayo hivi majuzi ilirejesha serikali ya eneo la kabla ya vita huko Tigray baada ya kuvunja utawala wa muda wa kikanda ulioanzishwa chini ya Mkataba wa Pretoria, imeishutumu serikali ya shirikisho kwa kuhujumu makubaliano hayo.

    Ukiwa umetiwa saini nchini Afrika Kusini mwaka 2022 ili kumaliza vita vya Tigray vilivyodumu kwa miaka miwili, mkataba huo "umeshindwa kwa kiasi kikubwa kufanya kazi," taarifa hiyo ilibainisha, na kuongeza kuwa hakuna masharti yake ya msingi ambayo yametekelezwa ipasavyo.

    Kulingana na TPLF, vikosi vya Ulinzi vya kitaifa vya Ethiopia vimeanzisha uhamasishaji mkubwa wa kijeshi kwenye mipaka ya Tigray, kuzunguka eneo hilo na kusababisha shida kubwa ya kijamii na kiuchumi na dhiki ya kisaikolojia miongoni mwa wakazi wake.

    Pamoja na mivutano hiyo, TPLF ilisisitiza dhamira yake ya kupata suluhisho kwa njia ya amani.

    Kundi hilo liliwahimiza wahusika wa kimataifa kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuleta pande zote kwenye meza ya mazungumzo. "Hali hiyo inahitaji hatua za haraka, zilizoratibiwa na madhubuti ili kuanzisha mazungumzo ya kisiasa ya kuaminika kabla ya kuchelewa," taarifa hiyo ilionya.

    Iliongeza kuwa vita tayari vinaharibu maeneo ya Amhara na Oromia, na hatari ya makabiliano mapya yanayohusisha Tigray "inazidi kuongezeka."

  4. Wachunguzi Zanzibari wasema mwanamitindo wa Marekani Ashlee alijiua

    .

    Chanzo cha picha, social

    Polisi huko Zanzibar wamehitimisha kuwa mshawishi wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, Ashley Robinson, mwenye umri wa miaka 31, alifariki kwa kujiua kufuatia msongo wa mawazo, baada ya uchunguzi kuhusu kifo chake katika hoteli moja visiwani humo.

    Bi Robinson, ambaye pia alijulikana kama Ashlee Jenae, alifariki baada ya tukio lililotokea katika hoteli moja kisiwani huko tarehe 8 mwezi wa Aprili.

    Akitoa taarifa kuhusu matokeo ya uchunguzi huo Alhamisi, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Zuberi Chembera, alisema wachunguzi wamebaini bila shaka kwamba kifo cha Bi Robinson kilitokana na kujiua na kwamba hakuna mtu mwingine aliyehusika.

    "Kupitia maelezo ya mashahidi na uchunguzi wa vifaa vya mawasiliano vya marehemu na mchumba wake, tulibaini kuwa alikuwa na msongo wa mawazo. Ujumbe waliotumiana ulionyesha malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na hali ya maisha yake," Chembera aliwaambia waandishi wa habari mjini Zanzibar.

    Tukio hilo lilizua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuibuka kwa taarifa zinazokinzana kuhusu mazingira ya kifo chake.

    Katika matokeo yake ya awali, polisi walisema Robinson alijitoa uhai kufuatia kutofautiana na mchumba wake, Joseph McCann, 45. Hata hivyo, ripoti zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa huenda ndiye aliyemuua.

    Polisi baadaye walianzisha uchunguzi kamili na kuchukua pasipoti ya McCann na kumhoji kama sehemu ya taratibu za kawaida.

    Kulingana na wachunguzi, McCann na Bi Robinson waliingia katika jumba la kifahari la Zuri Hotel tarehe 6 Aprili na kutoelewana kulitokea kati ya wanandoa hao karibu saa sita mchana tarehe 8 Aprili, na kusababisha mzozo ambao haujatatuliwa.

    Wasimamizi wa hoteli waliarifiwa na kumhamisha McCann hadi Villa 65 huku juhudi zikiendelea kushughulikia hali hiyo.

    Polisi walisema alipatikana akiwa amejilingalinga kwenye chuma cha kutundika nguo kwa kutumia mkanda wa nguo unaotolewa kwa kawaida kwa wageni katika vyumba vya hoteli.

    Familia ya mshawishi na McCann hazijatoa maoni kuhusu matokeo ya polisi wa Zanzibar.

    Bi Robinson na McCann walikuwa wamesafiri hadi Tanzania kwa likizo na kusherehekea siku yake ya kuzaliwa tarehe 5 Aprili.

    Alimchumbia siku hiyo hiyo, siku nne kabla ya kifo chake.

    Mwili wa Bi Robinson baadaye ulirudishwa Marekani tarehe 24 Aprili, na ibada ya mazishi yake ilifanyika Mei 05 huko New Jersey.

    Soma zaidi:

  5. Chanjo ya 'kwanza duniani' iliyoundwa na Akili mnemba

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Akili mnemba imetumika kutengeneza aina ya chanjo "mpya" ambayo inaweza kuwa kinga dhidi ya idadi kubwa ya virusi na kuzuia magonjwa ya mlipuko, wasema watafiti.

    Timu katika Chuo Kikuu cha Cambridge inasema ni mara ya kwanza kwa sehemu muhimu ya chanjo kubuniwa kikamilifu na AI na kisha kujaribiwa kwa watu.

    Chanjo hiyo ilibuniwa ili kufanya kazi kwenye virusi vyote vya korona ambavyo vingejumuisha aina zote za Covid na virusi vinavyoambukiza wanyama, lakini pia vinaweza kuanzisha janga.

    Bado iko katika hatua za mwanzo, lakini timu tayari inatengeneza chanjo tofauti ambazo zinaweza kukabiliana na mafua na Ebola.

    Chanjo hufundisha miili yetu jinsi ya kugundua maambukizi ili kuongeza nafasi zetu za kupambana nayo.

    Lakini baadhi ya virusi vina ujuzi wa kubadilisha mwonekano wao - au kubadilika - kwa hivyo chanjo zinaweza kushindwa kufanyakazi haraka. Ndiyo maana chanjo za Covid na homa ya majira ya baridi zinahitaji kusasishwa mara kwa mara.

    "Siku zote tuko nyuma," alisema Profesa Jonathan Heeney, kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, akiongeza kuwa "tunachojaribu kufanya ni kuwa mbele" na hadi sasa kuna uwezo wa kujikinga dhidi ya milipuko mipya au magonjwa ya mlipuko.

    Soma zaidi:

  6. Shule Kenya hazitafungwa mapema kwa likizo ya katikati ya muhula - Waziri

    .

    Chanzo cha picha, Shutterstock

    Katibu wa Wizara ya Elimu Kenya Prof. Julius Bitok ameondoa uwezekano wa shule kufungwa mapema kwa ajili ya mapumziko ya katikati ya muhula huku ghasia zikiendelea kushuhudiwa katika shule mbalimbali kote nchini.

    Waziri alisema wizara ya elimu imeingilia kati kwa ushirikiano na washikadau ili kujua tatizo liko wapi na kurejesha hali ya utulivu na kuongeza kuwa zaidi ya 90% zinaendelea na ratiba zao kama kawaida.

    Shule kadhaa zilizoathirika zimelazimika kufungwa kwa muda na kuongeza wasiwasi huku wanafunzi wa shule ya utumishi wanaoshukiwa kuchoma bweni na kusababisha vifo vya wenzao 16 wakiamriwa kuendelea kusalia rumande.

    Soma zaidi:

  7. Wananchi washambulia timu ya mazishi DRC, hofu ya Ebola kuenea yaongezeka

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), zimeeleza wasiwasi mkubwa baada ya wakazi wa eneo la Katana katika jimbo la Kivu Kusini kushambulia timu maalum ya mazishi ya waathirika wa Ebola.

    Tukio hilo lilitokea Jumatatu na kulazimisha wahudumu wa afya kuacha jeneza walilokuwa wakilisafirisha kutokana vurugu hizo.

    Kwa mujibu wa taarifa za wizara ya afya, mwili wa marehemu uliendelea kushughulikiwa na wananchi wa kawaida baada ya timu hiyo kuondoka. Hatua hiyo inatajwa kuwa hatari kubwa kwa sababu miili ya waathirika wa Ebola inaweza kuendelea kusambaza maambukizi ikiwa haitashughulikiwa kwa kufuata taratibu maalum za afya.

    Tukio hilo limeongeza changamoto katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa aina ya Bundibugyo ya Ebola, huku kukiwa na taarifa za mashambulizi mengine dhidi ya wahudumu wa afya na timu za mazishi katika maeneo tofauti. Katika mji wa Bunia, jimbo la Ituri, watu kadhaa walijeruhiwa baada ya wakazi kushambulia timu ya wahudumu wa afya kwenye makaburi.

    Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa ukosefu wa imani kutoka kwa baadhi ya wananchi na upinzani dhidi ya hatua za kudhibiti ugonjwa huo vinaendelea kuathiri mapambano dhidi ya Ebola. Baadhi ya familia zimekuwa zikipinga taarifa rasmi za sababu za vifo vya ndugu zao, jambo linalochochea migogoro na wahudumu wa afya.

    Tangu mlipuko huu wa 17 wa Ebola nchini DRC kutangazwa Mei 15, jumla ya wagonjwa 363 wamethibitishwa kuambukizwa huku watu 62 wakifariki dunia. Maambukizi yameendelea kuongezeka katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, hali inayoongeza hofu ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huo ikiwa hatua za kudhibiti maambukizi hazitaheshimiwa kikamilifu.

  8. Tetesi za soka: Diomande, Kroupi wazigonganisha Arsenal, PSG na Liverpool

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Arsenal wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Mabingwa wa Ulaya, Paris Saint-Germain, (PSG) katika harakati za kumsajili mshambuliaji Mfaransa Eli Junior Kroupi kutoka Bournemouth, pamoja na mshambuliaji wa Argentina Julian Alvarez anayechezea katika Atletico Madrid. (Independent)

    Liverpool inamtaka winga wa Ivory Coast, Yan Diomande, baada ya kuwasiliana na klabu ya RB Leipzig. Hata hivyo, klabu hiyo ya Ujerumani ina msimamo wa kutomuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19. (Athletic)

    PSG pia wanamfuatilia Diomande. Inadaiwa kuwa mchezaji huyo mwenyewe angependa zaidi kuhamia PSG kuliko sehemu nyingine yoyote. (Telefoot, via Mirror)

    Beki wa Chelsea, Marc Cucurella, anaangalia uwezekano wa kuondoka Stamford Bridge, huku Atletico Madrid ikijiandaa kutoa ofa yake ya kwanza kwa ajili ya nyota huyo wa Hispania. (Teamtalk)

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Brentford wamepeleka dau la £43m kwa ajili ya kumsajili winga wa Mjerumani Said El Mala kutoka FC Cologne. (Bild) Hata hivyo, El Mala hana nia ya kuhamia klabu hiyo ya Ligi Kuu England. (Sky Sports Germany)

    Juventus wanahitaji angalau £26m ili kumuachia beki wa pembeni wa Italia Andrea Cambiaso, ambaye anahusishwa pia na vilabu vya Chelsea na Barcelona. (Calciomercato)

    Mshambuliaji wa Serbia, Dusan Vlahovic ataondoka Juventus mwishoni mwa mwezi Juni baada ya kuamua kutosaini mkataba mpya na klabu hiyo ya Italia. (Football Italia)

    Juventus wameonyesha tena nia kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta. (Gazzetta dello Sport)

  9. Zelensky apendekeza mazungumzo ya ana kwa ana na Putin ili kumaliza vita vya Ukraine

    Z

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ametoa wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati yake na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika juhudi mpya za kutafuta suluhisho la kumaliza vita vinavyoendelea kati ya nchi hizo mbili.

    Kupitia barua ya wazi aliyomwandikia Putin, Zelensky alisema kuwa ni muhimu viongozi hao wawili kukutana moja kwa moja ili kujadili njia za kurejesha amani.

    Katika barua hiyo yenye zaidi ya maneno 1,800, Zelensky alisisitiza kwamba amani ya kudumu inaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Ukraine na Urusi. Aliongeza kuwa haitakuwa sahihi kusubiri hadi Marekani irejee kuipa kipaumbele vita vya Ulaya baada ya kuelekeza nguvu zake kwenye migogoro mingine ya kimataifa, ikiwemo suala la Iran.

    Zelensky pia alipendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa kipindi chote cha mazungumzo hayo ili kutoa mazingira mazuri ya kufikia makubaliano. Hata hivyo, Putin awali alikataa wazo la kusitisha mapigano kwa muda, akisisitiza kuwa bado kuna masuala muhimu yanayohitaji kujadiliwa kabla ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote.

    Serikali ya Urusi imethibitisha kupokea barua hiyo na kusema kwamba rais wa Urusi atapewa taarifa kamili kuhusu yaliyomo kabla ya kutoa msimamo rasmi.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, pia alitoa maoni yake kuhusu pendekezo hilo, akisema kuwa itakuwa jambo jema ikiwa viongozi hao wawili watakutana uso kwa uso. Wakati huo huo, Zelensky alipendekeza kwamba mazungumzo hayo yaweze kufanyika katika nchi isiyoegemea upande wowote kama Switzerland au Turkey.

    Vita kati ya Urusi na Ukraine vilianza kwa uvamizi mkubwa wa Urusi mwezi Februari mwaka 2022 na vimesababisha maelfu ya vifo pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu. Licha ya majaribio kadhaa ya mazungumzo yaliyofanyika katika maeneo mbalimbali, juhudi za kufikia usitishaji wa mapigano zimekuwa zikikwama. Pendekezo hili jipya la Zelensky linaonekana kuwa hatua nyingine muhimu katika kutafuta njia ya kumaliza mzozo huo wa muda mrefu.

  10. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Juni 5, 2026