Mapendekezo 3 ya kodi yanayozua utata miongoni mwa Wakenya

Ni picha ya awali ya wakati wa mswada wa fedha wa 2024

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Mapendekezo ya muswada wa fedha 2024 yalizua maandamano na kushurutisha Rais Ruto afute baadhi ya vipengee
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Kwa wiki kadhaa sasa, Muswada wa Fedha wa mwaka 2026 umekuwa kitovu cha mjadala nchini Kenya. Mitandao ya kijamii imejaa madai kuwa muswada huo utaongeza gharama za maisha, utaanzisha kodi mpya za ardhi na hata kubadilisha umiliki wa kudumu wa ardhi kuwa umiliki wa muda maalum.

Hata hivyo, si kila taarifa inayosambazwa mtandaoni ni sahihi.

Bunge la Kenya limesema wazi kuwa Muswada wa Fedha wa mwaka 2026 hauna kifungu chochote kinachohusu ardhi, kodi ya ardhi au kubadilisha umiliki wa kudumu kuwa umiliki wa muda maalum.

"Muswada wa Fedha wa mwaka 2026 una jumla ya vifungu 57, na hakuna hata kimoja kinachohusu ardhi," ilisema taarifa hiyo ya bunge la Kenya.

Badala yake, mjadala halisi unahusu mapendekezo kadhaa ya kodi ambayo yanaweza kuathiri matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali, magari ya umeme, kuongeza mamlaka ya KRA katika ukusanyaji wa kodi na baadhi ya sekta za biashara.

Je, Miamala ya majukwaa ya kidijitali itakuwa ghali zaidi?

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Suala linalojadiliwa zaidi na Gen Z wa kenya ni pendekezo la kutozwa ushuru wa thamani yaani VAT wa asilimia 16 kwa majukwaa ya malipo ya kidijitali ya M-Pesa, Airtel Money na Pesapal.

Muswada unapendekeza kuondoa msamaha wa VAT uliokuwa ukitumika kwa baadhi ya huduma za kifedha za kidijitali. Serikali inasema VAT itatozwa kwa watoa huduma wanaowezesha miamala hiyo.

Hata hivyo, mwanachama wa kamati ya ushuru na fedha za umma Caleb Mokaya ameonya kuwa gharama hizo huenda zikahamishiwa watumiaji kupitia ada za juu za miamala, jambo litakalowaathiri watumizi wa kipato cha chini wanaotegemea huduma hizo.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wadau katika muungano wa sekta ya kibinafsi KEPSA wamesema mapendekezo hayo yanaweza kufanya mifumo ya malipo ya kidijitali ishindwe kujiendesha kifedha, kuwafanya wafanyabiashara kurejea katika miamala ya fedha taslimu isiyo rasmi, na kudhoofisha mafanikio yaliyopatikana chini ya Mkakati wa Kitaifa wa Malipo wa mwaka 2022 hadi 2025.

Kwa mujibu wa Safaricom, gharama za miamala zinaweza kuongezeka kwa asilimia 33.4 kutokana na mchanganyiko wa VAT na ushuru wa bidhaa maalum.

Kwa mfano, kodi ya VAT kwa uhamishaji wa dola 38.60 kupitia huduma ya M-Pesa ingeongezeka kutoka kiwango cha sasa cha sifuri hadi Shilingi 9.12 pesa za Kenya iwapo mapendekezo hayo yataidhinishwa kama yalivyo.

Makampuni ya Safaricom, Airtel Kenya pamoja na wataalamu wa kodi kutoka KPMG, PwC na RSM yanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kuwafanya wananchi wenye kipato cha chini na biashara ndogo ndogo kubeba mzigo mkubwa zaidi wa gharama za miamala.

Kwa upande wake, Hazina ya Taifa ya Kenya inasisitiza kuwa muswada haujaanzisha kodi mpya inayolenga moja kwa moja miamala ya fedha kwa simu.

Vile vile, Waziri wa Hazina ya Taifa nchini humo John Mbadi ametetea wazo hilo akisema kuwa VAT inapaswa kutozwa kwa watoa huduma wanaowezesha miamala.

Mabadiliko ya ushuru wa simu za kisasa

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Serikali inasema inalenga kupunguza mzigo wa ushuru kwa simu kutoka asilimia 55 hadi asilimia 25 kwa kuunganisha ushuru uliopo sasa. Nao wakenya wameonekana kutoamini pendekezo la serikali wakilitaja kuwa ni danganya toto na yanaweza kupotosha kuhusu gharama halisi ya simu.

Kwa mfano, ukinunua simu za kisasa eneo la duka la jumla na mwenzako anunue katika duka la hapo mtaani kwa shilingi elfu ksh 20,000 na ksh25,000 mtawalia pesa za kenya caleb amehoji asilimia ya ushuru itawekwa kwa kiasi gani maalum ya bei ya simu. Kutokana na hilo mchambuzi wa mswada wa fedha aliyezungumza na BBC Swahili ameeleza hiyo itakuwa kizungumkuti kwa serikali na kwa wanunuzi wa simu ambazo ndizo hutumika katika maongezi ya kila siku nchini Kenya.

Muswada huo pia unajumuisha pendekezo lingine lisilohusiana moja kwa moja ambalo linaweza kuwanufaisha Wakenya wanaosafiri nje ya nchi na wanaohitaji kununua, kutoa zawadi au kuboresha simu zao za mkononi.

Kiwango cha thamani ya bidhaa ambazo wasafiri wanaoingia Kenya kutoka nje ya nchi wanaweza kuingiza bila kutozwa ushuru kinapendekezwa kuongezwa kutoka dola 300 za Marekani (takriban shilingi 39,000 za Kenya) hadi dola 2,000 za Marekani (takriban shilingi 260,000 za Kenya).

Hii ina maana kuwa wasafiri wataweza kurejea nchini na bidhaa nyingi zaidi za matumizi binafsi, zawadi na bidhaa nyingine bila kutozwa ushuru, mradi thamani yake isizidi kiwango kipya kilichopendekezwa.

Magari ya umeme yanaweza kuwa ghali zaidi

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Pendekezo ambalo kamati ya bunge ya fedha inapaswa kutathmini kabla ya kuidhinisha kuwa sheria ni kuweka ushuru kwa magari, betri na pikipiki zinazotumia umeme.

Kipengee hicho kikipitishwa kama kilivyo gharama ya kununua vifaa vinavyotumia umeme pekee itaongezeka kwani watengenezaji hawatoweza kurejesha ushuru wa thamani kwa malighafi waliotumia.

Kwa sasa baadhi ya bidhaa hizi zimekuwa zikifaidika na misamaha ya kodi ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa ushuru aliyezungumza na BBC Swahili, iwapo mapendekezo hayo yatapitishwa, gharama za kuagiza au kutengeneza baadhi ya vifaa vya usafiri wa umeme zinaweza kuongezeka

Wadau wa mazingira wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kupunguza kasi ya mpito wa Kenya kuelekea matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.

Serikali ya Ruto inataka KRA iwe na nguvu gani zaidi?

Katika suala la KRA, pendekezo likaloruhusu mamlaka ya kodi kutumia taarifa zilizokusanywa na taasisi za kifedha na makampuni ya mawasiliano ili kukadiria ni kiwango gani unapaswa kulipa kodi limekereketa wakenya wengi.

Wataalamu wa ushuru wamesema kuwa mfumo huo umekosa uwazi na iwapo utapitishwa kuwa sheria mamlaka hiyo itakuwa na nguvu ya kujua pesa unazozipata kwa akaunti yako ya pesa na itakuwa inakiuka sheria ya usiri wa data.

''Mamlaka ya kukusanya ushuru ikiwa na nguvu ya kupata taarifa za siri za watu itakuwa inakiuka faragha ya raia wa Kenya na hilo haikubaliki kisheri'', anasema Caleb Mokaya.

Wanaounga mkono hatua hiyo wanasema itasaidia kupunguza ukwepaji wa kodi.

Wanaopinga wanaona inaweza kuongeza wasiwasi kuhusu faragha ya taarifa za kifedha za wananchi.

Kwa sasa, sheria inaruhusu KRA kuunganisha mifumo yake na ya biashara, lakini inakataza kufikia data za kibinafsi.

Wakenya wanaoishi nje ya nchi wataathirikaje?

Muswada huo unapendekeza kuanzishwa kwa Kifungu cha 6B katika Sheria ya Kodi ya Mapato ili kuweka utaratibu wa kutoza kodi kwa watu wanaoishi nje ya Kenya lakini wanapata mapato kutokana na nyumba zao za kupangisha nchini.

Muswada pia unapendekeza kodi ya mwisho ya asilimia 10 kwa watu wanaoishi nje ya Kenya lakini wanapata mapato kutokana na nyumba zao za kupangisha nchini.

Masharti hayo hayatatumika pale ambapo mapato ya nyumba yanapokelewa kupitia wakala mkazi nchini na tayari yanatozwa kodi ya zuio (withholding tax) kwa mujibu wa kifungu cha 35(3)(j) cha Sheria ya Kodi ya Mapato.

Mswada huo pia unafafanua "mtu asiye mkazi" kuwa ni mtu aliye nje ya Kenya.

Kwa mfano, ikiwa Mkenya anayeishi Uingereza anamiliki nyumba Nairobi na anapata Sh100,000 kwa mwezi kutokana na upangishaji, atalipa Sh10,000 kama kodi.

Serikali inasema lengo la pendekezo hilo ni kurahisisha ukusanyaji wa kodi kutoka kwa wamiliki wa nyumba wanaoishi nje ya nchi.

Vipengee ambavyo havikuwekwa kwa mswada

Rais wa Kenya William Ruto aliwahi kupendekeza kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya wafanyakazi (PAYE) kwa asilimia 5, lililokuwa limefungamanishwa na msamaha wa kodi kwa mapato ya kwanza ya hadi Shilingi elfu 30,000 za Kenya kwa mwezi, limeondolewa kwa sasa ili kufanyiwa tathmini zaidi.

Wakati huo huo, pendekezo la ushuru wa zuio (withholding tax) kwenye ada za miamala ya kadi za malipo linalenga kuziba mianya ya kisheria iliyobainishwa katika maamuzi ya awali ya mahakama.

Kuna kizuri ndani ya mswada wa fedha mpya?

Ndio.

Japokuwa ni sehemu ndogo ya watu wanaounga mkono mswada wa fedha wa mwaka huu kuna masuala ambayo mtaalamu wa masuala ya ushuru Caleb Mokaya ameyaeleza yataleta nafuu kwa wananchi wa kawaida.

Kwanza kabisa, muswada unapendekeza kuondoa kodi kwenye mafao ya pensheni yanayolipwa kwa familia baada ya kifo cha mnufaika.

Pili, unapendekeza kupunguza baadhi ya adhabu kwa walipa kodi wanaochelewa kuwasilisha marejesho yao ya kod kwa mamlaka ya KRA na pia kupunguza faini ya kulipa kwa walipa ushuru waliochelewa.

Tatu, kiwango cha bidhaa ambazo msafiri anaweza kuingiza nchini bila kulipa ushuru kinapendekezwa kuongezwa kutoka takribani Sh39,000 hadi Sh260,000 pesa za Kenya.

Hatua hiyo inaweza kuwanufaisha Wakenya wanaosafiri nje ya nchi na kurejea na bidhaa za matumizi binafsi au zawadi.

Mpango wa serikali ya Kenya wa kuongeza mapato mwaka ujao kuanzia Julai yaani Mswada wa Fedha wa 2026 umeelezwa na wachanganuzi wa uchumi kuwa unaonekana kuepuka hatua kali za ushuru kama zile za Mswada wa Fedha wa 2024 ulioondolewa kufuatia maandamano ya kitaifa yaliyosababisha vifo vya vijana kadhaa.

Propaganda kuhusu mswada wa fedha ni zipi?

Baadhi ya wakenya haswa walioko mitandaoni wameendelea kutafsiri vibaya baadhi ya vipengee wakiamini kuwa muswada huo utaongeza gharama za maisha kwa kila mtu, ilhali mapendekezo yake yanatofautiana kulingana na sekta na aina ya kodi inayohusika.

Nakala ya muswada wa fedha wa mwaka huu iliyosomwa na BBC Swahili hakuna ushuru mpya kwa mkate kama inavyoenezwa mitandaoni.

Kuhusu pendekezo la kuhamisha tarehe ya mwisho ya kuwasilisha marejesho ya kodi ya mapato kutoka Juni 30 hadi Aprili 30. Ingawa hatua hiyo imekosolewa na baadhi ya watu, ukisoma kwa kina mswada huo lengo lake ni kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kuoanisha ratiba ya kodi ya Kenya na viwango vya kimataifa.

Kwa upande wa biashara ya mitumba, baadhi wanadai muswada unapendekeza kuipiga marufuku, bali kwa tafsiri ya mtaalamu wa ushuru aliyozungumza na BBC Swahili unapendekeza ushuru wa VAT katika uagizaji wa bidhaa hizo pamoja na kodi nyingine zinazoweza kuathiri bei zake sokoni.

Kinachoonekana wazi ni kwamba Muswada wa Fedha wa mwaka 2026 una mchanganyiko wa mapendekezo yanayoweza kuongeza gharama katika baadhi ya sekta na mengine yanayolenga kurahisisha mfumo wa kodi au kutoa nafuu kwa makundi fulani ya wananchi.

Kinachoibuka ni kuwa muswada huo ambao ulichapishwa kwa gazeti la serikali mwezi Mei tarehe 5 mwaka huu ni nakala ambayo sio rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuuelewa kutokana na wingi wa ukurasa wa 124 na maneno yaliyohitaji uelewa wa sheria.

Kipi kinachofuata?

Muswada wa fedha 2026 umetamatisha mchakato wa ukusanyaji maoni ya wananchi tarehe 24 mwezi mei 2026 sasa hatua inayofuata ni muhimu kwani bunge linapaswa kutathmini mapendekezo yaliyotolewa na wadau pamoja na raia.

Kibarua kigumu kiko mbele ya bunge ambapo watahitajika kuchuja mapendekezo na kunyoosha mswada huo uendane na vipau mbele vya kiuchumi vya nchi.

Hata hivyo, kiongozi wa upinzani Kenya, Kalonzo Musyoka, amewataka Wakenya kuupinga Muswada wa Fedha wa mwaka 2026 katika hali yake ya sasa, akidai kuwa una vipengele vya siri vinavyoweza kuwaongezea wananchi mizigo ya kifedha kupitia mikataba ya upangishaji wa muda mrefu.

"Ukataliwe Muswada wa Fedha wa mwaka 2026/27 katika hali yake ya sasa kwa sababu unaelekea kuanzisha kwa njia ya kificho mikataba ya upangishaji ambayo itawaathiri kwa kiasi kikubwa wakenya wakipato cha chini," alisema Kalonzo.

Aidha, aliwaambia wakenya kuwa muswada huo, haujatoa suluhisho kwa changamoto za kiuchumi zinazowakabili Wakenya, bali unaongeza mzigo kwa wananchi ambao tayari wanakabiliwa na ugumu wa maisha.