Moja kwa moja, Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya, Kuwait yasema uwanja wa ndege umeshambuliwa na Iran
Mashambulizi ya hivi karibuni yanatokea baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.
Muhtasari
- Kwa picha: Ziara ya Rais Samia nchini Urusi
- Wahamiaji 180 wa Nigeria warejeshwa nyumbani kutoka Libya kwa msaada wa IOM
- Trump asema Mojtaba Khamenei anahusika pakubwa katika mazungumzo na Marekani
- Ukraine yashambulia St Petersburg huku kongamano la kiuchumi la Putin likifunguliwa
- Wanafunzi wanaoshukiwa kuchoma bweni la shule Kenya kuzuiliwa rumande kwa siku 21
- Shell iliendesha bomba la mafuta Nigeria licha ya kujua kuwa inachafua mazingira
- Ndege isiyo na rubani yashambulia basi katika eneo linalodhibitiwa na Urusi nchini Ukraine
- Mamlaka Uhispania yapiga marufuku mechi ya kirafiki na DR Congo kwa hofu ya Ebola
- Upinzani wataka raia kususia kutoka nje ishara ya kupinga jaribio la kurekebisha Katiba DRC
- Marekani yawawekea vikwazo waasi wanaohusishwa na serikali ya DRC na Rwanda
- Muswada wa kuongeza muda wa rais wa Zimbabwe wapita hatua ya kwanza ya usomaji bungeni
- Israel yashambulia kusini mwa Lebanon
- Tetesi za Soka Ulaya: Aston Villa haina mpango wa kumuuza Rogers
- Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Ambia Hirsi
Kwa picha: Ziara ya Rais Samia nchini Urusi

Chanzo cha picha, IKULU
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameanza ziara ya siku tatu nchini Urusi kuanzia Juni 3 hadi 5, 2026, ambapo atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, pamoja na kushiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026).

Chanzo cha picha, IKULU

Chanzo cha picha, IKULU
Maelezo ya picha, Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Samia nje ya Bara la Afrika, tangu vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 
Chanzo cha picha, IKULU
Soma zaidi:
Wahamiaji 180 wa Nigeria wanarejea nyumbani kutoka Libya kwa msaada wa IOM
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM limesema wahamiaji 180 wa Nigeria wakiwemo wanawake na watoto wamerejea nyumbani kutoka Libya baada ya safari ngumu katika njia za wahamiaji.
Walifika Jumanne usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed wa Lagos wakiwa ndani ya ndege ya kukodi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji lilisema lilifanya kazi na serikali ya Nigeria na kwa usaidizi wa Umoja wa Ulaya, kuwasaidia wanaorejea "kwenye hali ya kawaida".
Wengi wa waliokuwa kwenye meli walikuwa wamezuiliwa katika vituo vya Benghazi, Libya, kabla ya kurejea Nigeria kwa hiari.
IOM ilisema kundi hilo lilijumuisha wanawake watu wazima 108 na wanaume watu wazima 45, pamoja na watoto.
Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya shirika hilo, ugumu wa kiuchumi unasalia kuwa kichocheo kikuu cha uhamiaji nchini Libya, huku 77% ya wahamiaji waliohojiwa wakitaja ukosefu wa kazi na mapato duni nyumbani.
Ripoti yake ya Matrix ya Ufuatiliaji wa Uhamisho pia ilibainisha wahamiaji nchini Libya kutoka nchi 29 za Afrika, wengi wao kutoka Afrika Magharibi na Kati.
Niger inachangia 51%, Chad 25%, na Nigeria 9% - kwa pamoja wanaunda 85% ya idadi ya wahamiaji kutoka eneo hilo.
Trump asema Mojtaba Khamenei anahusika pakubwa katika mazungumzo na Marekani

Chanzo cha picha, GETTY
Maelezo ya picha, Rais Trump na kiongozi wa Iran Mojtaba Khamenei Rais Donald Trump amesema Iran imekubali kutounda silaha za nyuklia.
Rais wa Marekani pia alisema Mojtaba Khamenei anahusika katika mazungumzo na Marekani.
Bw. Trump aliambia podikasti ya "Pod Force One" kuhusu kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu: "Ningependa kukutana naye na pengine tutakutana wakati fulani, kulingana na ikiwa kila kitu kitaenda sawa."
Rais wa Marekani alisema ana imani kuwa Mojtaba Khamenei alihusika katika mazungumzo hayo na Marekani na kwamba ingawa hajisikii vizuri, amethibitisha mazungumzo hayo.
Pia aliita suala la Iran "mafanikio makubwa": "Tutaona kitakachotokea. Tunashughulikia makubaliano, na ikiwa yatafanikiwa, ni bora. Ikiwa hayatafanikiwa, ni sawa. Tutafanya kwa njia nyingine."
Bw. Trump pia alikiri kwamba alikuwa na mazungumzo makali na Benjamin Netanyahu: "Ndiyo, nilifanya. Nisingesema nilikuwa na hasira, lakini nilisikitishwa kidogo na vita vyake vya mara kwa mara na Lebanon."
Rais wa Marekani alisema anaelewana vyema na Waziri Mkuu wa Israel.
Tovuti ya habari ya Axios iliripoti jana kuwa Donald Trump alimpigia simu Benjamin Netanyahu akimuita"mwendawazimu" katika simu Jumapili usiku: "
Una... wazimu. Kama si mimi, ungekuwa jela sasa hivi... kila mtu anakuchukia hivi sasa. Kila mtu anachukia Israeli kwa sababu ya hili."
Ripoti hii ilikuwa na sauti kubwa sana, haswa nchini Israeli.
Soma zaidi:
Ukraine yashambulia St Petersburg huku kongamano la kiuchumi la Putin likifunguliwa

Chanzo cha picha, Reuters
Ukraine imefanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani viungani mwa mji wa St Petersburg nchini Urusi, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa kongamano kuu la kiuchumi linalolenga kuwavutia wawekezaji wa kigeni nchini humo.
Kulipopambazuka moshi mweusi ulitanda katika mji wa pili wa Urusi, ambapo Vladimir Putin anatarajiwa kuhutubia hafla ya kifedha siku ya Ijumaa.
Maelfu ya wageni kutoka nchi 130 wanatarajiwa kuhudhuria, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa ngazi ya chini wa Marekani.
Mamlaka za eneo hilo zilisema kuwa walinzi wa anga walidungua ndege 59 zisizo na rubani usiku kucha na kwamba wilaya tatu tofauti za St Petersburg zilipigwa, ingawa hakuna mtu aliyeuawa.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema Moscow itajibu shambulio hilo.
"Majibu yetu yatakuwa ya kimfumo," alisema Jumatano. Mtandao wa simu ulitatizwa na Uwanja wa Ndege wa Pulkovo mjini St Petersburg ulifungwa kwa muda, huku baadhi ya maeneo ya karibu ya Latvia na Estonia pia yakitoa arifa kuhusu uvamizi wa anga.
Pia unaweza kusoma:
Habari za hivi punde, Wanafunzi wanaoshukiwa kuchoma bweni la shule Kenya kuzuiliwa rumande kwa siku 21

Chanzo cha picha, Analodu via Getty Images
Mahakama mmoja nchini Kenya amewapa wachunguzi siku 21 kuwazuilia wanafunzi tisa wanaohusishwa na mkasa wa moto wa bweni katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Utumishi na kusababisha vifo vya wanafunzi 16.
Wanafunzi hao, ambao utambulisho wao haujafichuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto, watasalia rumande ya watoto hadi uchunguzi utakapokamilika.
Hakimu Mkuu Abdulqadir Lorot alisema wapelelezi wanachunguza uwezekano wa mashtaka ya mauaji na uchomaji moto, na kuyataja kama makosa makubwa yanayohitaji uchunguzi wa kina.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa muda wa ziada unahitajika ili kukamilisha vipengele muhimu vya uchunguzi.
Waendesha mashtaka pia walielezea wasiwasi kuwa kuwaachilia washukiwa kunaweza kuvuruga ushahidi.
Mawakili wa utetezi walipinga ombi hilo wakisema kwamba hakukuwa na sababu za msingi za kuendelea kuwazuilia wanafunzi hao.
Mahakama hata hivyo imewaruhusu watoto hao kutembelewa na mawakiliwa wao wakiwa kizuizini.
Kesi hiyo iliendeshwa chini ya udhibiti vikali, ukijumuisha utangazaji wa moja kwa moja wa matukio kwa sababu washukiwa ni watoto.
Kesi hiyo itatajwa Juni 24 katika Mahakama ya Naivasha.
Soma zaidi:
Watu 21 wafariki kwenye mkasa wa moto Delhi

Chanzo cha picha, Reuters
Takriban watu 21 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya moto kuzuka katika jengo la ghorofa katika mji mkuu wa India Delhi, polisi wamesema.
Baadhi ya waathiriwa walikuwa raia wa kigeni kutoka nchi za Kusini mwa Asia ambao walikuwa nchini India kwa matibabu au wameandamana na jamaa zao wanaopokea huduma ya matibabu, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.
Jengo hilo linadaiwa kutoa huduma ya makazi kwa wagonjwa na jamaa za wale wanaopokea matibabu katika hospitali ya kibinafsi iliyo karibu.
Zaidi ya watu 40 waliokolewa na kupelekwa hospitalini.
Bado haijabainika ni watu wangapi walikuwa ndani ya jengo hilo katika eneo la Malviya Nagar moto ulipozuka.
Chanzo cha moto huo pia hakijajulikana.
Wazima moto wamefanikiwa kuudhibiti moto huo, huku shughuli za uokoaji zikiendelea katika eneo hilo.
Waziri wa Delhi Ashish Sood alisema viongozi walikuwa wakichunguza ikiwa jengo hilo lilikuwa na idhini ya kutoa huduma ya makazi, na kuongeza kwamba wale watakaopatikana na hatia ya ukiukaji wowote watakabiliwa na uhalifu.
Waziri Mkuu Narendra Modi ametoa rambirambi zake na kutangaza fidia ya dola 2,088 za Kimarekani kwa familia za waliofariki na rupia 50,000 kwa waliojeruhiwa.
Marekani yatangaza ushuru mpya kudhibiti ajira ya lazima

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani imetangaza ushuru mpya wa 10-12.5% dhidi ya mataifa kadhaa kwa kutofanya vya kutosha kukabiliana na ajira ya kulazimishwa.
Ni mara ya pili kwa utawala wa Rais Donald Trump kutangaza ushuru mpya wa bidhaa kutoka nje tangu Mahakama ya Juu ya Marekani kufuta majukumu yake ya awali mwezi Februari.
Washirika 60 wa biashara walioorodheshwa - ikiwa ni pamoja na Uingereza, Umoja wa Ulaya(EU), Canada, na Japan - wanachangia karibu bidhaa zote zinazouzwa kwa Marekani.
Idara ya Biashara ya Marekani ilisema nchi hizi zitakabiliwa na ushuru huo kwa sababu ya kushindwa kushughulikia uagizaji wa bidhaa zinazokuzwa kupitia ajira ya kulazimishwa.
Wakosoaji wanasema sera ya Trump ya ushuru imesababisha kupanda kwa bei nchini Marekani na kwingineko.
Msimamo wa serikali ya Marekani ni kwamba biashara na nchi zinazonunua vitu vilivyokuzwanywa kupitia watu kutummikishwa kwa lazima sio haki kwa Marekani.
Mwakilishi wa Biashara wa Marekani Jamieson Greer alisema "huleta mabadiliko ambapo wafanyakazi wa Marekani wanalazimishwa kushindana kimataifa kwenye uwanja usio na usawa".
Uamuzi wa ushuru unakuja baada ya Marekani kuanza uchunguzi mwezi Machi kuhusu washirika 60 wa kibiashara, ambao wanajumuisha 99.4% ya bidhaa za Marekani zinazoagizwa kutoka nje, kwa kuhofia kuendekeza ajira ya lazima.
Soma pia:
Shell iliendesha bomba la mafuta Nigeria licha ya kujua kuwa inachafua mazingira

Chanzo cha picha, Simi Jolaoso / BBC
Kampuni ya kimataifa ya Uingereza ya mafuta Shell iliendelea kuendesha bomba kubwa la mafuta nchini Nigeria kwa miaka mingi ingawa ilijua ilikuwa ikisababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira - licha ya onyo kutoka kwa wafanyakazi wake na viwango vyake vya kiufundi, nyaraka za ndani zilizopatikana na kipindi cha BBC zinaonyesha.
Faili hizo, ikiwa ni pamoja na barua pepe na mawasilisho, zinaonyesha kwamba mtendaji mkuu wa Shell alionya mapema mwaka wa 2008 kuhusu hatari za kuendeleza mradi wa mamilioni ya mapipa ya mafuta yasiyosafishwa kupitia mojawapo ya mabomba makuu ya kampuni hiyo Afrika, huku ikikabiliwa na wizi mkubwa na uharibifu usiodhibitiwa na miundombinu.
Kote katika eneo la kusini mwa Niger Delta lenye utajiri wa mafuta nchini Nigeria, miongo kadhaa ya umwagikaji wa mafuta umeacha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kwenye mandhari husika, huku maeneo yenye unyevunyevu yakizidi kufunikwa na mashapo yaliyochafuliwa.
BBC ilipata nyaraka hizo za ndani baada ya kampuni ya Shell kuzifichua kama sehemu ya kesi zinazoendelea nchini Uingereza zilizoletwa na jamii zinazoishi karibu na vijito na mikoko ya Niger Delta, ambazo zinataka kampuni ya Shell iwajibike kwa uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na uvujaji zaidi ya 100 wa mafuta unaotokana na wizi na usafishaji haramu wa bidhaa hiyo kati ya 2011 na 2013 ambao umeathiri afya zao, mazingira na riziki zao za kila siku.
Bomba hilo, ambalo Shell ililiuza mwaka jana, lilikuwa moja ya miundombinu yake mikubwa, ya gharama kubwa zaidi na hatimaye yenye matatizo zaidi nchini Nigeria.
Lilikuwa na uwezo wa kubeba hadi mapipa 150,000 ya mafuta kwa siku, lakini lilikumbwa mara kwa mara na uvujaji wa mafuta na kulengwa na wezi haramu wa mafuta.
Katika karatasi za mahakamani, kampuni ya mafuta inasema kwamba uchafuzi mwingi umesababishwa na "wizi mkubwa wa mafuta, hujuma" na viwanda vingi vya kusafisha mafuta haramu, na kwamba kampuni yake tanzu ya Nigeria iliwekeza sana kwa miaka mingi ili kupunguza hatari na kukabiliana na kuvuja kwa mafuta.
Pia unaweza kusoma:
Ndege isiyo na rubani yashambulia basi katika eneo linalodhibitiwa na Urusi nchini Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Watu saba wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia basi la abiria lililokuwa likisafiri kupitia sehemu inayodhibitiwa na Urusi ya Ukraine, afisa mmoja alisema.
Denis Pushilin, kiongozi aliyeteuliwa na Urusi wa eneo la mashariki mwa Donetsk nchini Ukraine, alisema basi hilo lilishambuliwa mapema Jumatano lilipokuwa likisafiri kati ya Moscow na Simferopol, katika eneo la Crimea inayokaliwa na Urusi.
Urusi ilidondosha zaidi ya ndege zisizo na rubani 350 usiku kucha, kulingana na maafisa wa Urusi.
Hii inafanyika siku moja baada ya shambulio kubwa la Urusi katika miji kote Ukraine na kuua watu wasiopungua 22, wakiwemo wanawake na watoto kadhaa.
"Huko Yenakiyevo, ndege isiyo na rubani ilishambulia basi la Moscow-Simferopol; kulingana na ripoti za awali, raia saba waliuawa," Pushilin alisema katika chapisho la Telegram Jumatano.
Aliongeza kuwa watu 11 waliojeruhiwa walikuwa wakipokea huduma za kimatibabu.
Maafisa waliongeza kuwa ndege zisizo na rubani zilidondoshwa katika maeneo ya Belgorod, Kursk na maeneo mengine ya magharibi, pamoja na karibu na Moscow na katika Bahari ya Azov.
Takriban ndege zisizo na rubani 50 zilidondoshwa katika eneo la Leningrad kaskazini magharibi mwa Moscow, kulingana na gavana wa eneo hilo Alexander Drozdenko.
Pia unaweza kusoma:
Mamlaka Uhispania yapiga marufuku mechi ya kirafiki na DR Congo kwa hofu ya Ebola

Chanzo cha picha, Getty Images
Mamlaka ya Uhispania imefuta mechi ya maandalizi ya kandanda kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Chile kabla ya Kombe la Dunia, kutokana na wasiwasi wa kuenea kwa virusi vya Ebola.
Juan Franco, Meya wa La Linea de la Concepcion kusini mwa Uhispania ambapo mchezo wa Juni 9 ulipangwa kufanyika, alisema alitia saini amri ya kupiga marufuku mechi hiyo.
"Ripoti ya mkuu wa huduma ya afya ya meya wa La Línea ilishauri dhidi ya kuandaa mechi kutokana na hatari za kiafya ambazo zinaweza kutokea," alisema.
Bw. Franco pia alielezea hatua hiyo kama tahadhari.
Hata hivyo, katika taarifa yake siku ya Jumanne, Chama cha Soka cha Congo kilisema timu hiyo imefuata kanuni zote muhimu za afya na michezo kuhusiana na mchezo huo wa kirafiki.
"Kwa sasa majadiliano yanaendelea na mamlaka husika, Shirikisho la Soka la Uhispania, pamoja na vyombo husika vya kimataifa, ili kupata suluhu la haraka na muafaka," taarifa hiyo iliongeza.
Kufuzu kwa DRC kwa Kombe la Dunia - la kwanza katika zaidi ya miaka 50 - kulipokelewa kwa furaha na matumaini. Hata hivyo, mlipuko wa virusi vya Ebola mwezi Mei uligeuza hadithi yao ya furaha kuwa moja ya kutokuwa na uhakika, hofu, na msukosuko.
Kambi yao ya kwanza ya mazoezi mjini Kinshasa ilifutwa na kuhamishiwa Ubelgiji kutokana na hofu ya Ebola. Wafuasi kutoka nchini pia walikabiliwa na vizuizi vya kusafiri na visa kwa baadhi ya nchi mwenyeji kwa sababu ya hofu za kiafya.
Soma zaidi:
Upinzani wataka raia kususia kutoka nje ishara ya kupinga jaribio la kurekebisha Katiba DRC

Chanzo cha picha, Reuters
Viongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamewataka wananchi kushiriki katika mgomo wa kutotoka mijini leo Jumatano, ili kupinga kile wanachokieleza kuwa ni vitisho dhidi ya Katiba ya nchi hiyo.
Hatua hiyo inakuja wakati bunge likijadili mswada wa kura ya maoni, ambao wachambuzi wanasema unaweza kufungua njia ya uwezekano wa kuongeza muda wa utawala wa Rais Félix Tshisekedi.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Viongozi mashuhuri wa upinzani kama vile Moïse Katumbi na Martin Fayulu walioshika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia katika uchaguzi wa rais wa 2023, wanasema wanapinga jaribio lolote la kubadilisha katiba ya sasa, ambayo inaruhusu mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.
Katika matamko tofauti, waliwataka raia kukaa nyumbani Jumatano, na kuongeza kwamba shule, majengo ya biashara na huduma za umma zinapaswa kufungwa kama kielelezo cha wao kupinga.
"Mtu yeyote asitoke nje, ili kuonesha kwamba tunapinga ukoloni wa nchi yetu, mabadiliko ya Katiba, na kukataa kuruhusu mtu kubaki madarakani milele," Fayulu alisema katika ujumbe wa video kwa wafuasi wake.
Mamlaka za DRC ziliwataka watu - hasa watumishi wa umma - kutotii wito kama huo wa kususia.
"Wasimamizi na wafanyakazi ambao, katika kipindi husika...hawapo wenyewe kwenye vituo vyao vya kazi bila uhalali watakabiliwa na sheria kwa mujibu wa kanuni zinazotumika," Jean-Pierre Lihau Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Utumisi wa Umma alisema katika taarifa kwa umma.
Pia alisisitizia uhitaji wa watumishi wa umma kutoegemea upande wowote kisiasa na kutopendelea.
Mwezi uliopita, Rais Felix Tshisekedi alisema yuko tayari kugombea muhula wa tatu iwapo "wananchi wanataka" abaki. Alisema ili hilo lifanyike, kutahitajika marekebisho ya katiba baada ya kura ya maoni. Rais pia alipendekeza kwamba mzozo wa mashariki mwa nchi unaweza kusababisha kucheleweshwa kwa uchaguzi wa 2028, na kuzua hasira miongoni mwa upinzani.
Wengi wanasema anapanga mkakati wa kusalia madarakani, huku wabunge wa upinzani wakiondoka kwenye kikao cha bunge cha Mei 27, kilichokusudiwa kujadili muswada wa kura ya maoni.
Kilichosalia ni kusubiri kuona iwapo watu wataitikia miito ya upinzani.
Pia unaweza kusoma:
Muswada wa kuongeza muda wa rais wa Zimbabwe wapita hatua ya kwanza ya usomaji bungeni

Chanzo cha picha, Getty Images
Muswada tata ambao unaweza kuongeza muda wa urais nchini Zimbabwe umepita hatua yake ya kwanza ya usomaji bungeni.
Sheria hiyo inayopendekezwa inalenga kurekebisha katiba ili kuongeza muda wa muhula wa rais na wabunge kutoka miaka mitano hadi saba.
Pia unalenga kubadilisha mfumo wa uchaguzi wa rais, ambapo badala ya kura ya moja kwa moja ya wananchi, bunge litakuwa na mamlaka ya kumchagua kiongozi wa nchi.
Utasomwa mara ya pili Jumatano wakati wabunge watakapojadili uhalali wa marekebisho zaidi ya kumi.
Ibara zenye utata zaidi zinapendekeza kuruhusu Rais Mnangagwa na wabunge kusalia ofisini hadi 2030 na kubadilisha kura ya urais kutoka kwa mchakato wa umma hadi wa bunge.
Marekebisho yaliyopendekezwa yamesababisha ghadhabu kwa wananchi na yanakabiliwa na changamoto kadhaa za kisheria.
Wakosoaji wakiwemo Chama cha Wanasheria nchini humo wanasema mapendekezo hayo yanadhoofisha taasisi za kidemokrasia na kulimbikiza madaraka kwa rais.
Makanisa makubwa na mashirika ya haki za binadamu wanasema mabadiliko hayo ni kinyume na katiba na yanahitaji kura ya maoni.
Mswada huo utahitaji angalau theluthi mbili ya kura katika Mabunge yote mawili ili kupitishwa.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yawawekea vikwazo waasi wanaohusishwa na serikali ya DRC na Rwanda

Chanzo cha picha, Reuters
Marekani imewawekea vikwazo makamanda wawili wa makundi yenye silaha wanaotuhumiwa kuchochea ghasia na ukosefu wa utulivu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne, Ofisi ya Idara ya Hazina ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni (OFAC) iilimwekea vikwazo Gustave Kubwayo, iliyemtambua kama kamanda wa kitengo cha kijasusi na operesheni maalum cha Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR).
Wakati huo huo, John Imani Nzenze, aliyesemekana kuwa kamanda na mkuu wa upelelezi wa kundi la waasi la M23 pia aliwekewa vikwazo.
"FDLR na M23 wameteka maeneo kwa kutumia nguvu na kuua raia mashariki mwa DRC," taarifa kutoka Idara hiyo ilisema.
Iliongeza kuwa: "Kutokana na hatua ya leo, mali na maslahi yote katika mali ya watu waliotambuliwa au waliozuiwa walioelezwa hapo juu ambazo ziko Marekani au katika milki au udhibiti wa watu wa Marekani zimezuiwa."
Rwanda inaishutumu serikali ya DRC kwa kuunga mkono FDLR, kundi lenye silaha lililoundwa na wanajeshi wa zamani wa Rwanda na watu wenye itikadi kali ambao walikimbilia mashariki mwa Congo wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994. Kigali inawachukulia waasi hao kuwa tishio.
Kwa upande mwingine, mamlaka ya Congo na waangalizi wengine wa kimataifa wameishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23, kundi lenye silaha ambalo limeteka maeneo mengi kutoka kwa serikali ya DRC katika kipindi cha mwaka uliopita.
"Ghasia zinazoendelea kufanywa na makundi yenye silaha zinazidisha mzozo mbaya wa kibinadamu na ni tishio kwa maslahi ya Marekani katika eneo hilo," Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema.
"Vikwazo vya leo vinaunga mkono azimio la amani na kukomesha umwagaji damu," aliongeza, akizitaka DRC na Rwanda kusitisha uungaji mkono wao kwa makundi yenye silaha yaliyoidhinishwa kama ilivyoainishwa na mikataba ya amani inayoongozwa na Marekani iliyotiwa saini mwezi Desemba mwaka jana.
Hii si mara ya kwanza kwa wanachama wa makundi yenye silaha nchini DRC kuwekewa vikwazo. Lakini hatua hizo zimeshindwa kukomesha mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo lenye machafuko.
Soma zaidi:
Tetesi za Soka Ulaya: Aston Villa haina mpango wa kumuuza Rogers

Chanzo cha picha, Getty Images
Aston Villa haina mpango wa kumuuza Morgan Rogers huku klabu kadhaa zikiwa na nia ya kumsajili kiungo huyo mshambuliaji, Barcelona bado wana hamu ya kumsajili Marcus Rashford kutoka Manchester United na Real Madrid wanafanya mazungumzo na beki wa kulia wa Inter Milan Denzel Dumfries.
Aston Villa wanajua kuwa kuna nia ya kumsajili kiungo mshambuliaji Morgan Rogers kutoka klabu kadhaa, ikiwemo Arsenal, lakini hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 23. (Telegraph - subscription required)
Beki wa pembeni wa Eintracht Frankfurt, Nathaniel Brown, mwenye umri wa miaka 22, ndiye anayewindwa na Bayern Munich na Arsenal. (The Athletic - subscription required)
Manchester City na Chelsea wanamtaka beki wa pembeni wa Juventus Andrea Cambiaso, 26, huku Barcelona pia ikifuatilia hali ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Italia. (Gazzetta dello Sport - in Italian)

Chanzo cha picha, Getty Images
Liverpool na Paris St-Germain huenda zote zikamtaka winga wa RB Leipzig Yan Diomande lakini klabu hiyo ya Ujerumani haitikiswi na hali hiyo kwani inaamini mchezaji huyo wa miaka 19 hataendelea kuwa nao kwa mwaka mwingine tu bali pia atasaini mkataba mpya ulioboreshwa. (Sky Sports Germany)
Kocha wa Barcelona Hansi Flick, mkurugenzi wa michezo Deco na rais Joan Laporta bado wana hamu ya kumsajili mshambuliaji wa Manchester United Marcus Rashford kwa mkataba wa kudumu huku Bayern Munich, Newcastle, Tottenham na Aston Villa wakimtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 28. (The I)
Juventus wanaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth na Uholanzi Justin Kluivert mwenye umri wa miaka 27 kama mbadala wa mchezaji wa Real Madrid mwenye umri wa miaka 26 wa Morocco Brahim Diaz. (Gazzetta dello Sport - in Italian)
Manchester United wamemfuatilia mlinzi wa Juventus na Ufaransa Pierre Kalulu na klabu ya Turin huenda ikalazimika kumuuza mchezaji huyo wa miaka 25 ili kusawazisha masuala ya miamala baada ya kushindwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa. (Corriere dello Sport - in Italian)
Kiungo wa kati wa Ureno Mateus Fernandes, 21, ameruhusiwa kuondoka West Ham baada ya mawasiliano kutoka Manchester United na Arsenal, huku Liverpool na Paris St-Germain pia zikimfuatilia. (Teamtalk)
Aston Villa, Atletico Madrid na Borussia Dortmund zinamtaka mshambuliaji wa Club Brugge, Mjerumani Nicolo Tresoldi, 21, baada ya msimu mzuri Ubelgiji. (The Athletic - subscription required)
Real Madrid wamefanya mazungumzo na mlinzi wa Inter Milan Denzel Dumfries, ambaye kima chake cha kuuza ni pauni milioni 21.6, huku wakimwona mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 30 kama shabaha yao kuu ya kuimarisha safu yao ya beki wa kulia. (Athletic)
Pia unaweza kusoma:
Israel yashambulia kusini mwa Lebanon

Chanzo cha picha, Reuters
Israeli imeendelea na mashambulizi yake kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne, lakini haikushambulia Beirut kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kiasi fulani na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Lebanon ilisema kwamba, chini ya makubaliano yaliyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump usiku wa Jumatatu, vikosi vya Israeli havitashambulia mji mkuu kwa mabomu nayo Hezbollah haitashambulia Israeli.
Hii ilitokea baada ya Iran kusema kwamba hatua ya Israeli nchini Lebanon inahatarisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyake na Marekani.
Kufuatia tangazo la kusitisha mapigano, jeshi la Israeli lilisema limezuia makombora mawili yaliyorushwa kaskazini mwa Israeli.
Hezbollah ilisema imeshambulia vikosi vya Israeli kusini mwa Lebanon, ambapo maafisa waliripoti mashambulizi mabaya ya Israeli.
Soma zaidi:
Marekani na Iran zaanzisha mashambulizi mapya huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama

Chanzo cha picha, X/US Central Command
Jeshi la Marekani linasema limeanzisha mashambulizi ya "kujilinda" dhidi ya Iran na kudungua makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani kwenye meli na nchi za Ghuba.
Mashambulizi hayo kwenye Kisiwa cha Qeshm, katika Mlango-Bahari wa Hormuz, yalikuwa "kujibu majaribio ya mashambulizi ya Iran kote Mashariki ya Kati", Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom) ilisema.
Iran ilisema imeshambulia kambi na helikopta za Marekani katika "nchi ya kikanda" kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani kama kulipiza kisasi.
Centcom ilisema Tehran imerusha makombora mawili dhidi ya Kuwait na matatu dhidi ya Bahrain, ambayo yote yalivunjika vipande vipande au kuzuiliwa.
Mashambulizi ya hivi karibuni yanatokea huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama, baada ya mazungumzo kuhusu makubaliano ya kukomesha vita vyao vya miezi kadhaa kushindwa kuendelea mwishoni mwa juma.
Centcom iliongeza kuwa shambulio hilo katika Kisiwa cha Qeshm lilikuwa limelenga kituo cha udhibiti wa ardhini cha jeshi la Iran, na kwamba jeshi la Marekani pia lilidungua ndege tatu zisizo na rubani ambazo zilikuwa zimerushwa na Iran kuelekea kwa "mabaharia raia waliokuwa wakipitia maji ya kikanda kihalali".
IRGC ilisema "kuvuruga usalama wa Mlango-Bahari wa Hormuz kutakuwa na gharama kubwa kwa jeshi la Marekani lenye uchokozi".
Iran imekuwa ikishambulia mara kwa mara maeneo ya Bahrain na Kuwait, ambapo kambi za kijeshi za Marekani zipo.
Hapo awali, Centcom ilisema imeishambulia na kuiharibu meli ya mafuta isiyo na mizigo iliyokuwa ikielekea Iran, kama sehemu ya kizuizi cha majini cha Washington kwenye Mlango-Bahari wa Hormuz.
Soma zaidi:
Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara tarehe ni 03/06/2026.










