Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Afrika kuanza kutumia Su-34M, ndege mpya za kivita za Urusi
Afrika imeingia katika hatua mpya ya ushindani wa kijeshi baada ya kuibuka kwa taarifa za kuwasili kwa ndege za kivita za Urusi aina ya Su-34M katika kikosi cha anga cha Algeria.
Hatua hiyo imezua mjadala mpana kuhusu iwapo bara hilo linaingia kwenye awamu mpya ya mbio za silaha, huku mataifa kadhaa yakiendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kivita.
Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanasema ujio wa ndege hizo hauwezi kuangaliwa kwa mtazamo wa nchi moja pekee, bali kama sehemu ya mabadiliko ya kimkakati yanayoendelea Afrika Kaskazini na bara zima. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mataifa mengine pia yanaimarisha vikosi vyao vya anga na mifumo ya makombora, hali inayoongeza ushindani wa kijeshi katika eneo hilo.
Kwa sasa, Su-34M inaonekana kuwa moja ya alama mpya za ushawishi wa kijeshi wa Urusi barani Afrika, hasa katika nchi zinazotegemea zaidi silaha zake za anga.
Swali kubwa linaloulizwa ni kama ujio wa ndege hizi utabadilisha kwa kiasi kikubwa uwiano wa nguvu za kijeshi au ni sehemu nyingine ya mzunguko wa kawaida wa biashara ya kisasa ya silaha duniani?
Su-34M ni ndege za aina gani?
Su-34M ni ndege ya kivita ya Urusi ambayo ni ya mashambulizi ya masafa marefu , iliyotengenezwa kwa ajili ya mashambulizi ya ardhini, baharini na pia kujilinda angani.
Ndege hii hutengenezwa na kampuni ya Sukhoi chini ya shirika la serikali la UAC (United Aircraft Corporation) nchini Urusi.
Ingawa msingi wake ni Urusi, Su-34M imekuwa sehemu ya mpango mkubwa wa usafirishaji wa silaha za Urusi kwa washirika wake wa kijeshi. Hata hivyo, bado matumizi yake makubwa yako ndani ya jeshi la anga la Urusi, ambapo imekuwa ikitumika katika operesheni mbalimbali za kijeshi katika miaka ya hivi karibuni.
Kuhusu Afrika, Algeria inaonekana kuwa miongoni mwa nchi chache za kwanza barani humo kupokea au kuhusishwa moja kwa moja na ndege hizi za kisasa. Hii inaifanya kuwa tukio la kipekee, kwani nchi nyingi za Afrika bado zinategemea zaidi ndege za vizazi vya zamani au mifumo ya magharibi na Urusi ya awali kama MiG na Su-30.
Kwa ujumla, upatikanaji wa Su-34M unaashiria hatua ya juu ya ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na baadhi ya mataifa ya Afrika, lakini bado si mwelekeo wa bara zima kwa sasa.
Su-34M ina uwezo gani wa kijeshi?
Su-34M imeundwa kwa ajili ya operesheni za mashambulizi ya mbali dhidi ya maeneo ya kimkakati, ikiwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa wa silaha ikiwemo mabomu ya kawaida na pamoja na makombora ya masafa marefu. Inaweza kufanya safari ndefu bila kujazwa mafuta mara kwa mara, hali inayoiwezesha kufikia malengo ya mbali.
Ndege hii pia ina mifumo ya kisasa ya rada na vita vya kielektroniki, inayoiwezesha kukwepa au kupunguza ufanisi wa mifumo ya ulinzi ya adui. Aidha, ina uwezo wa kufanya operesheni katika mazingira magumu ya hali ya hewa, jambo linaloipa unyumbufu mkubwa wa kijeshi.
Kwa upande wa muundo wake, Su-34M ina nafasi ya marubani wawili wanaokaa pamoja, tofauti na ndege nyingi za kivita za kawaida, jambo linalosaidia urahisi wa uratibu wakati wa misheni ndefu. Hii inafanya iwe bora zaidi kwa operesheni za muda mrefu za mashambulizi ya kimkakati.
Kwa ujumla, uwezo wake unaifanya kuwa moja ya ndege za mashambulizi zenye nguvu zaidi katika daraja lake, hasa inapounganishwa na mifumo ya kisasa ya Urusi ya ulinzi na mawasiliano ya kijeshi.
Su-34M zinaweza kubadilisha mizani ya nguvu ya kijeshi Afrika?
Ujio wa Su-34M barani Afrika unaongeza mjadala kuhusu kasi ya mbio za silaha, hasa Afrika Kaskazini ambako mataifa kama Morocco, Algeria na Misri yamekuwa yakiongeza uwekezaji mkubwa wa kijeshi. Kila upande unaimarisha uwezo wake wa anga, makombora na ulinzi wa anga kwa lengo la kujilinda na kuongeza ushawishi wa kikanda.
Kwa sasa, mataifa kama Misri hutumia ndege za F-16, Rafale na MiG-29, wakati Morocco imewekeza katika F-16 zilizoboreshwa na ina uhusiano wa karibu wa kijeshi na Marekani na Israel. Hii inaonyesha kwamba Afrika Kaskazini tayari ina mchanganyiko wa teknolojia za kijeshi za Magharibi na Urusi.
Ikilinganishwa na Su-34M, ndege nyingi za Afrika bado ziko katika daraja la ndege za kizazi cha nne, huku Su-34M ikiwa ni ndege zilizoboreshwa zaidi na za kisasa. Hii inaifanya kuwa na nafasi tofauti katika uwanja wa vita, badala ya kushindana moja kwa moja na ndege za F-16 au Rafale.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema kuongezeka kwa uwezo huu wa kijeshi kunaweza kuongeza tahadhari na mashindano ya silaha katika eneo hilo, lakini si lazima kubadili mizani ya nguvu kwa haraka. Badala yake, inaweza kuimarisha zaidi hali ya "usawa wa hofu" ambapo kila upande unaongeza uwezo wake bila kuvunja kabisa usawa na mizania iliyopo.