Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Hezbollah yapinga makubaliano mapya ya usitishaji vita kati ya Israel na Lebanon

Marekani ilitangaza makubaliano ya kusitisha mapigano Jumatano usiku kufuatia duru mpya ya mazungumzo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Hezbollah yapinga makubaliano mapya ya usitishaji vita kati ya Israel na Lebanon

    Kundi la wapiganaji la Hezbollah nchini Lebanon limepinga vikali masharti ya usitishaji vita kati ya Israel na Lebanon unaoungwa mkono na Marekani.

    Katika taarifa yenye maneno makali, kiongozi wa kundi linaloungwa mkono na Iran Naim Qassem alisema mazungumzo hayo "hayana msingi" na "ya kufedhehesha" kwa Lebanon, na kuongeza kuwa sehemu kubwa ya Welebanon "kinadharia" wanapinga mazungumzo haya.

    Kauli yake inajiri saa kadhaa baada ya Israel na Lebanon kutangaza upya usitishaji wa mapigano kwa makubaliana kwamba "Hezbollah watapigwa marufuku.

    Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Jumatano na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, nchi hizo tatu zilisema makubaliano hayo "yanategemea kusitishwa kabisa" kwa mashambulizi ya Hezbollah.

    Lakini akijibu siku ya Alhamisi, kiongozi wa Hezbollah - ambayo haikuwa sehemu ya mazungumzo - alisema "usitishaji mapigano unaotarajiwa", uliotafsiriwa na Israel kama Hezbollah kuweka chini silaha na kuwaondoa wapiganaji kutoka kusini mwa Lebanon ni sawa na kuslimu amri na hatua hiyo itatimiza malengo ya Israel.

    Kiongozi huyo Hezbollah pia alionya kwamba maadamu vijiji vya Lebanon vinashambuliwa kwa mabomu, eneo la kaskazini mwa Israel halitakuwa salama.

    Saa kadhaa kabla ya hapo, Rais wa Lebanon Joseph Aoun alitaja usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani kuwa fursa ya mwisho ya amani ya kudumu nchini Lebanon.

    Wakati huo huo Israel imesisitiza kuwa usitishaji vita hautazuia mashambulizi yake ya ardhini dhidi ya Hezbullah.

    Soma zaidi:

  3. Vita vya Iran: Trump awasuta wabunge waliopitisha azimio la kudhibiti mamlaka yake

    Rais wa Marekani Donald Trump amewasuta wabunge waliopiga kura ya kudhibiti mamlaka yake, akiwataja kuwa watu "wasio wazalendo".

    Siku ya Jumatano, Bunge la Wawakilishi la Marekani lilipitisha azimio la kumzuia Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi nchini Iran.

    Katika chapisho katika mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, rais huyo aliandika: "Jana Bunge lilipiga kura isiyo na maana ili kupunguza mamlaka yanya, nikiwa katika harakati za mwisho za kumaliza Vita na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ni nani angefanya jambo lisilo la kizalendo kama hilo?"

    Ikulu ya White House imepuuzilia mbali hatua hiyo.

    Pia imeelezea uamuzi huo kama jaribio lisilo la kikatiba la kudhibiti mamlaka ya rais.

    Kura hiyo ambayo iiliungwa mkono na wabunge 215 dhidi ya 208, ilikuwa ya kupitisha azimio la kudhibiti mamlaka ya kivita, ambalo lingemtaka Trump kuondoa majeshi ya Marekani au kutafuta idhini ya bunge kushughulikia mzozo huo.

    Endapo azimio hilo litapitishwa na Bunge la Seneti la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Republican, halitahitaji saini ya rais, ingawa inaweza kukabiliwa na changamoto ya kisheria.

    Chapisho la Trump Alhamisi asubuhi liliendelea kusema: "Wademocrat wanachochewa na chuki dhidi ya Trump.Wako tayari Nchi yetu ishindwe kuliko kunipa ushindi mwingine, miongoni mwa nyingine nyingi.''

    Soma zaidi:

  4. Israel: Operesheni za ardhini zitaendelea Lebanon licha ya makubaliano mapya ya kusitisha mapigano

    Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz anasema kuwa nchi hiyo itaendelea na operesheni zake za ardhini kusini mwa Lebanon kwa muda na kwamba wakaazi wa eneo hilo ambao wamefurushwa makwao na Israel hawataweza kurejea.

    Tamko lake linakuja siku moja baada ya Lebanon na Israel kutangaza kufikia makubaliano katika mazungumzo yaliyoandaliwa mjini Washington kujadili kuhusu utekelezaji wa usitishaji mapigano, ambao unashinikiza "kukomeshwa kabisa" kwa mashambulizi ya Hezbollah na kutimizwa kwa masharti mengine kadhaa.

    Katika taarifa yake leo, Bw. Katz alisema kuwa vikosi vya jeshi la Israel vitasalia katika maeneo maalumu kusini mwa Lebanon, ikiwa ni pamoja na eneo la Beaufort Castle, ngome ya miaka 900 ambayo Israel iliiteka siku ya Jumamosi.

    Alisema Israel itaendelea "kubomoa miundombinu ya kigaidi katika eneo hilo," huku "ikiwa na uhuru wa kuchukua hatua, kwa usaidizi wa Marekani, kushambulia Beirut kujibu mashambulizi dhidi ya jumuiya na maeneo ya Israel."

    Lebanon na Israel zilikubaliana siku ya Jumatano kusitisha upya mapigano chini ya mpango unaoungwa mkono na Marekani nchini Lebanon.

    Hapo awali walikuwa wamekubali kusitisha mapigano mwezi Aprili, na kuongezwa muda mwezi Mei, lakini mapigano yameendelea kushihudiwa.

    Pia unaweza kusoma:

  5. DR Congo yathibitisha mpango ya kuwarejesha nyumbani raia wake kutoka Afrika Kusini

    Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nchini Afrika Kusini umethibitisha kuwa raia wanaotaka kurejea nyumbani wanaweza kufanya hivyo chini ya mpango wa kuwarejesha makwao kwa hiari unaoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi.

    Maafisa wanasema jukumu la Ubalozi ni tu kuthibitisha uraia na kutoa hati za usafiri za muda, na kuongeza kuwa fomu ya kuwasilisha maombi inapatikana mtandaoni.

    Mamlaka zinasema kwamba ikiwa Serikali ya Congo itaanzisha hatua maalum kushughulikia suala hilo jamii itafahamishwa haraka iwezekananvyo.

    Wakongo wamehimizwa kuwa waangalifu, kuepuka makabiliano, kuheshimu sheria za Afrika Kusini, na kutegemea tu taarifa rasmi.

    Wakati huo huo, Ghana tayari imeanza kuwarejesha makwao raia wake.

    Takriban Waghana 300 walisafirishwa kwa ndege hadi Accra Mei 27, kundi la kwanza miongoni mwa takriban watu 800 waliosajiliwa kwa ajili ya kuhamishwa.

    Mamlaka inasema zaidi ya 1,500 wamejiandikisha, wakitaja wasiwasi wa usalama huku maandamano dhidi ya uhamiaji haramu ukiendelea.

    Siku ya Jumanne, serikali ya Malawi pia ilitangaza mipango ya kuwarejesha makwao raia walio tayari kutoka Afrika Kusini kufuatia maandamano yanayoendelea.

    Mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni ni tatizo kubwa nchini Afrika Kusini kwani mara nyingi wageni wanalaumiwa kwa ukosefu mkubwa wa ajira na uhalifu.

    Kuongeza mvutano huo, viongozi wa Vuguvugu la March & March wametangaza kwamba wageni wasio na vibali lazima waondoke Afrika Kusini ifikapo tarehe 30 Juni.

    Mratibu Sandile Dube alionya tarehe ya mwisho inapaswa kuzingatiwa, ingawa maafisa wanasisitiza kwamba utekelezaji wa masuala ya uhamiaji ni jukumu la serikali.

    Soma pia:

  6. Wabunge wa Zimbabwe kujadili Mswada wa kuongeza muhula wa urais madarakani

    Wabunge nchini Zimbabwe wanatarajiwa kuanza kujadili mswada tata utakaomfanya Rais Emmerson Mnangagwa kusalia madarakani kwa miaka miwili zaidi baada ya muhula wake madarakani kufikia kikomo.

    Wakosoaji wanasema pendekezo hilo ni kinyume cha sheria.

    Mvutano umekuwa ukiongezeka tangu mswada wa marekebisho ya katiba ulipoanza kusomwa bungeni wiki hii.

    Wabunge wanatazamiwa kuanza mjadala wao leo huku wengine wakidai wanakabiliwa na vitisho.

    Miongoni mwa vifungu vyenye utata katika mswada huo, ni pamoja na pendekezo la kuongeza muda wa sasa wa rais na bunge kwa miaka miwili - Na kuruhusu bunge kumchagua rais.

    Kamati ya pamoja ya bunge imesema zaidi ya asilimia 99 ya maoni yaliyopokelewa kutoka kwa umma yanaunga mkono mapendekezo hayo.

    Changamoto za kisheria zilizowasilishwa wiki hii, zinasema kwamba kura ya maoni inahitajika ili kuongeza muhula wa rais.

    Maelezo zaidi:

  7. Ukraine yatuhumiwa kwa mauaji ya wanne katika eneo la Crimea

    Mamlaka zinazoungwa mkono na Urusi katika eneo linalokaliwa la Crimea nchini Ukraine zimesema takriban watu wanne wameuawa katika wimbi la hivi punde la mashambulizi ya Ukraine kwenye rasi hiyo.

    Watu watatu waliuawa na saba kujeruhiwa katika moja ya mashambulizi katika kile kilichoelezwa kama "sehemu isiyo ya makazi" katika mji mkuu wa mkoa, Simferopol.

    Inaonekana kuwa shambulio la kwanza lililosababisha vifo huko.

    Katika tukio tofauti, mtu mmoja aliuawa na wengine watatu kujeruhiwa katika shambulio dhidi ya treni ya abiria iliyokuwa ikisafiri kuelekea mji wa Kerch, kiongozi wa Crimea aliyewekwa rasmi na Urusi alisema.

    Ukraine haijatoa tamko lolote. Ni siku ya tatu mfululizo Kyiv inatuhumiwa kulenga usafiri wa umma katika maeneo yake inayokaliwa.

    Hivi karibuni Ukraine imepanua mashambulizi yake ndani ya Urusi, pia.

    Siku ya Jumatano, ilifanya mashambulizi viungani mwa St Petersburg, saa chache kabla ya kufunguliwa kwa kongamano kuu la kiuchumi liliandaliwa kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini humo.

    Kwa mujibu wa Rais Volodymyr Zelensky, ndege zisizo na rubani za Ukraine zilishambulia maeneo kadhaa nchini Urusi, ikiwa ni pamoja na kituo cha mafuta na kambi ya jeshi la wanamaji katika mji wa karibu wa Kronstadt - kituo kikuu cha Meli ya Baltic ya Jeshi la majini la Urusi.

    Soma zaidi:

  8. Kufuatilia waathiriwa wa Ebola ni changamoto, juhudi zinaendelea kuimarika - WHO

    Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza Jumatano kwamba juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zinaendelea kuimarika, huku visa 344 vikithibitishwa na vifo 60 kuripotiwa.

    Hata hivyo, changamoto zinaendelea, hasa katika kuongeza uwezo wa kupima na kufuatilia waathiriwa.

    Mlipuko huo unaosababishwa na ugonjwa wa Bundibugyo, umeenea pia katika nchi jirani ya Uganda, ambapo maambukizi 15 yamethibitishwa, ikiwa ni pamoja na kifo kimoja.

    Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisisitiza kwamba wakati hatua inapigwa, mengi zaidi yanahitajika kufanywa, huku asilimia 45 tu ya mawasiliano ya wale waliokutana na waathiriwa ndiyo yanayofuatiliwa kwa sasa.

    Wakati huo huo, Dkt. Tedros Ghebreyesus, ameonya dhidi ya kuwekwa kwa vikwazo vya jumla vya usafiri na baadhi ya nchi kutokana na mlipuko wa unaoendelea wa virusi vya Ebola.

    Marufuku ya kusafiri yaliyowekwa na zaidi ya nchi kumi na mbili yanaathiri uwezo wa Shirika la Afya Ulimwenguni kukabiliana vilivyo na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

    Marufuku hiyo ya kusafiri "inatatiza usambazaji na kuzuia mwitikio wa kukabiliana na Ebola," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus aliambia mkutano wa waandishi wa habari.

    Wito wa Dkt. Tedros unakuja baada ya Idara ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia ya Canada kurejelea tena uamuzi wake wa kusitisha utoaji wa stakabadhi za uhamiaji kwa wakazi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Uganda na Sudan Kusini kwa muda wa siku 90.

    Marekani, Bahrain, Mexico na nchi zingine zimeweka vizuizi vya kusafiri, wakati Canada inatekeleza karantini ya siku 21 kwa wasafiri wote wanaofika kutoka Congo.

    Kando na hayo, WHO imesema inahitaji angalau dola milioni 115 katika kipindi cha miezi mitatu ijayo ili kukabiliana na dharura hiyo ya kiafya.

    Shirika hilo limeeleza kuwa hadi sasa limefanikiwa kupata takribani asilimia 35 ya fedha zinazohitajika.

    Soma zaidi:

  9. Kura ya Bunge la Ulaya ni utaratibu wa kawaida – Serikali ya Tanzania

    Serikali ya Tanzania imesema kuwa hatua ya kamati mbili za Bunge la Ulaya kupitisha mapendekezo kuhusu mpango wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya (EU) ni sehemu ya taratibu za kawaida za kibunge na si uamuzi wa mwisho.

    Katika taarifa yake kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania imesisitiza kuwa uamuzi uliofikiwa Juni 3, 2026 katika ngazi ya kamati hauwezi kutafsiriwa kama msimamo wa mwisho wa EU kuhusu uhusiano wake na nchi hiyo.

    Katika mfumo wa Umoja wa Ulaya, mamlaka ya kiutendaji yapo chini ya Tume ya Ulaya (European Commission), ambayo ndiyo inayosimamia utekelezaji wa sera na uhusiano wa kikanda, lakini yanaweza kuwa na athari katika maamuzi ya mwisho ya maazimio ya Bunge.

    Kwa mujibu wa wizara hiyo, mapendekezo yaliyopitishwa bado yanapaswa kuwasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha Bunge zima la Ulaya lenye zaidi ya wabunge 700, kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa mwisho.

    Tarehe 3 Juni, Kamati ya Mambo ya Nje na Kamati ya Maendeleo za Bunge la Ulaya zilifanya kura kuhusu mapendekezo yanayohusiana na Mpango wa Ushirikiano wa Maendeleo wa mwaka 2025 kati ya EU na Tanzania. Katika kura hiyo ya ngazi ya kamati, mapendekezo yalipitishwa kwa kura 81 za kuunga mkono, kura 1 ya kupinga na kura 4 za kutokujizuia.

    Serikali ya Tanzania imesisitiza kuwa uhusiano wake na EU bado uko imara na kwamba hatua hiyo ni sehemu ya michakato ya kawaida ya ndani ya Bunge la Ulaya.

    Hata hivyo, moja ya mapendekezo yaliyotolewa yanaweza kuathiri Tanzania endapo yatapitishwa na Bunge zima na baadaye kutekelezwa, ikiwemo uwezekano wa kusitishwa kwa msaada wa euro milioni 156.

    Baadhi ya hoja zilizotajwa katika mjadala kuelekea upigaji huo wa kura zinahusiana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na mwenendo wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

    Hata hivyo, Tanzania imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa uchaguzi wake ulikuwa huru na wa haki, na kwamba masuala ya ndani yanapaswa kushughulikiwa kupitia mifumo ya ndani bila kuingiliwa.

  10. Serikali haitashauriana na Wakenya juu ya kituo cha Ebola cha Marekani Kenya – Waziri wa Afya

    Waziri wa Afya wa Kenya Aden Duale amesema kwenye kikao cha Bunge kuwa Serikali haitashauriana na Wakenya juu ya mpango wa kujenga kituo cha Karantini cha wagonjwa wa Ebola wa Marekani.

    Ugonjwa huu hauhitaji mashauriano kabla ya Wakenya kuambukizwa. Sisi kama serikali tuna wajibu wa kimaadili kuwalinda Wakenya na watu wengine ambao si Wakenya wanaoishi ndani ya mipaka yetu au wanaosafiri ndani ya nchi yetu, amesema Duale.

    Waziri Duale alikuwa ameitwa na Bunge kuelezea utayari wa Kenya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao umelipuka katika nchi ya Kidemokrasi ya Congo.

    Akielezea jinsi ambavyo hali ya ugonjwa huu sio ya kawaida, alisema Sheria ya Afya ya Umma inaipa Wizara ya Afya Kenya jukumu la kuhakikisha usalama kwa umma

    Akizungumzia kituo cha Ebola kilichopendekezwa kujengwa huko kambi ya kijeshi ya Laikipia kwa ushirikiano na Marekani, Duale alisema kitahudumia raia wote ikiwa ni pamoja na Wakenya na ni miongoni mwa vituo vingine 23 vya Ebola ambavyo tayari vimejengwa au vinapangwa kujengwa kote nchini.

    Soma zaidi:

  11. Polisi Zimbabwe waonya kuwa kuchochea vurugu hakutavumiliwa

    Polisi nchini Zimbabwe wamewaonya wananchi dhidi ya kuchochea ghasia na vitisho kwenye mitandao ya kijamii huku mswada wa kuongeza muda wa Rais Emmerson Mnangagwa ukisomwa kwa mara ya pili bungeni, Jumanne.

    Polisi waliweka kizuizi njiani kuelekea bungeni mswada huo ukisomwa kwa mara ya pili katika Bunge la Kitaifa.

    Sheria inayopendekezwa itaongeza mihula ya urais na wabunge kwa miaka miwili na kufutwa kwa kura ya moja kwa moja ya urais kupigwa na umma.

    Waziri wa sheria alitetea mswada huo unaolenga kuongeza muhula wa urais na kufuta kura ya moja kwa moja ya urais akisema italeta utulivu wa kisiasa.

    Wakosoaji wanasema mapendekezo hayo ni kinyume cha sheria na yanadhoofisha demokrasia.

    Kundi la wapiganaji wa zamani wa vita vya ukombozi, mashirika ya kiraia na wananchi wamewasilisha changamoto za kisheria kuzuia mswada huo.

    Hata hivyo inatarajiwa kupitia Mabunge yote mawili ambapo chama tawala cha Zanu PF kinashikilia zaidi ya thuluthi mbili ya wabunge.

    Soma zaidi:

  12. Mapigano yanaendelea mjini Mogadishu kati ya upinzani na vikosi vya serikali

    Mapigano yaliyozuka Jumatano alasiri kati ya vikosi vilivyoungana na upinzani na wanajeshi wa serikali yaliendelea hadi Jumamosi asubuhi katika mji mkuu wa Somalia.

    Milio ya risasi iliripotiwa katika vitongoji kadhaa huku mapigano yakiendelea, kulingana na wenyeji.

    Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, akizungumza wakati wa machafuko hayo, alisema: "Ikiwa rais na wanajeshi wake wanafikiri kwamba tunaogopa au tutatoroka, hatutakimbia."

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, alisema ghasia hizo hazitasitisha maandamano yaliyopangwa katika mji mkuu.

    "Shambulio hili halitasitisha maandamano ya wakaazi wa mji mkuu wanaopinga dhuluma, kulazimishwa kuhama makazi yao, na matumizi mabaya ya mamlaka ya serikali."

    Jeshi la Polisi la Somalia pia limelaani shambulizi katika kituo cha ukaguzi wilaya ya Hawlwadaag, likiwalaumu watu waliotumia silaha.

    "Jeshi la Polisi la Somalia linalaani na kujutia sana shambulio lililofanywa leo na wanamgambo wenye silaha waliovalia barakoa kwenye kizuizi cha polisi katika wilaya ya Hawlwadaag. Wanamgambo hao pia walitumia silaha nzito wakati wa shambulio hilo."

    Kikosi hicho kiliongeza kuwa waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

    Machafuko hayo yanatokea huku kukiwa na mvutano mkubwa wa kisiasa na mkwamo wa juhudi za upatanishi zinazohusisha viongozi wa upinzani, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Hassan Ali Khaire na Rais wa zamani Sharif Sheikh Ahmed, pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Marco Rubio aonya juu ya 'hatari' ya kuongezeka kwa vita vya Ukraine

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuna hatari kubwa ya kuongezeka kwa mvutano katika vita kati ya Urusa na Ukraine.

    Bwana Rubio alieleza kamati ya Bunge kwamba hatari zimeongezeka kutokana na Ukraine kuwa na uwezo zaidi wa kufanya mashambulizi ndani kabisa ya eneo la Urusi.

    Amesisitiza kuwa Marekani iko tayari kuchukua jukumu lolote ili kusaidia kufanikisha amani, ikiamini kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huo, lakini akasema kuwa pande zote mbili bado haziko tayari kufanya makubaliano ya kuachana na vita.

    Aidha, Bwana Rubio ameongeza kuwa Marekani si mpatanishi huru katika mzozo huo, kwa kuwa inaendelea kuiuzia Ukraine silaha na pia kudumisha vikwazo dhidi ya Urusi.

    Soma zaidi:

  14. Wabunge wamgeuka Trump, wapitisha azimio la kuzuia vita dhidi ya Iran

    Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha azimio la kumzuia Rais Donald Trump kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran

    Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 215 dhidi ya 208, baada ya wabunge wanne wa Chama anachotoka Trump cha Republican kuungana na wale wa Democrats katika hatua ya nadra ya kupinga hadharani vita hivyo, kati ya Marekani na Iran vilivyoanza mwezi Februari.

    Hata hivyo, azimio hilo bado linahitaji kupitishwa na Bunge la Senate, linalodhibitiwa na Republican. Hata likipitishwa huko, Trump anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya veto kuzuia azimio hilo kuwa sheria, jambo ambalo linahitaji theluthi mbili ya kura katika mabunge yote mawili ili kubatilishwa.

    Wabunge wa Republican Thomas Massie, Brian Fitzpatrick, Tom Barrett na Warren Davidson waliungana na Democrats kuunga mkono azimio hilo. Barrett alisema ni jukumu la Bunge pekee kutangaza vita na kwamba alipiga kura kulingana na dhamiri yake, bila kujali shinikizo lolote la kisiasa.

    Mbunge Gregory Meeks wa Democrats alieleza kura hiyo kama pigo kubwa kwa Trump, akisema vita dhidi ya Iran vimekuwa vya gharama kubwa, havijafanikisha malengo yake yaliyotangazwa na vimeongeza ugumu wa kupata suluhisho la kidiplomasia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

    Pia alisema Republican wengi wanaanza kusikiliza wapiga kura wao ambao hawataki vita vingine vya muda mrefu Mashariki ya Kati.

    Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Marekani na Iran zimeendelea kushambuliana katika siku za karibuni.

    Akizungumza kutoka Ikulu ya White House, Trump alisema mazungumzo ya kumaliza vita yanaendelea vizuri na yanaweza kukamilika mwishoni mwa wiki hii, akiongeza kuwa pande zote ziko karibu kufikia makubaliano ya kumaliza mzozo huo.

  15. Tetesi za soka: Fernandes kusalia United? Jesus wa Arsenal kutua Everton

    Manchester United wameahirisha mazungumzo ya kuongeza mkataba wa nahodha wao na kiungo wa Ureno, Bruno Fernandes, mwenye miaka 31, baada ya kuhakikishiwa kuwa anataka kubaki Old Trafford kwa muda mrefu. (Mirror)

    Real Madrid wanatarajiwa kutoa pauni milioni 17.3 ili kumsajili beki wa kulia wa Inter Milan na timu ya taifa ya Uholanzi, Denzel Dumfries, mwenye miaka 30. (Sky Sports)

    Everton wanamuwania mshambuliaji wa Brazil wa Arsenal, Gabriel Jesus, mwenye umri miaka 29, lakini wanataka mabingwa hao wa Ligi kuu kupunguza bei yao ya pauni milioni 20. (Football Insider)

    Paris Saint-Germain wanataka euro milioni 30 (pauni milioni 25.9) kutoka Juventus kwa ajili ya mshambuliaji wa Ufaransa mwenye miaka 27, Randal Kolo Muani. (La Gazzetta dello Sport)

    Atletico Madrid wanaweza kutumia fedha watakazopata kutokana na mauzo ya mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, mwenye miaka 26, kumsajili mshambuliaji wa Marseille na England, Mason Greenwood, mwenye miaka 24. (Fichajes)

    Roma pia wanamfuatilia Mason Greenwood, huku klabu yake ya zamani Manchester United ikitarajiwa kunufaika kupitia kipengele cha asilimia ya mauzo ya baadaye kilichowekwa wakati wa uhamisho wake kwenda Ufaransa. (Teamtalk)

    AC Milan wanamtaka Crysencio Summerville, mwenye umri wa miaka 24, kutoka West Ham United. Winga huyo wa Uholanzi pia anafuatiliwa na Tottenham Hotspur na Aston Villa. (Teamtalk)

  16. Israel na Lebanon zakubaliana kusitisha mapigano Hezbollah ikisitisha mashambulizi

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetangaza katika taarifa kwamba Israel na Lebanon zimekubaliana kutekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Makubaliano hayo "yanatokana na kukomeshwa kabisa" kwa mashambulizi kutoka kwa kundi lenye silaha la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, miongoni mwa masharti mengine.

    Hii inafuatia mashambulizi ya Israel kuua watu wasiopungua tisa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatano na Hezbollah kufyatua makombora kaskazini mwa Israeli, ikiwa majaribu makubwa katika makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa hapo awali mwezi Aprili.

    "Nchi zote zilithibitisha tena kwamba mustakabali wa uhusiano kati ya Israeli na Lebanon lazima uamuliwe na serikali mbili huru. Zilikataa jaribio lolote, la serikali yoyote au mhusika yeyote asiye wa serikali, kushikilia siku zijazo za Lebanon," ilisema taarifa hiyo.

    Makubaliano hayo pia yanategemea "kuwahamisha wanajeshi wote wa [Hezbollah]" kutoka eneo ambalo Israeli inadhibiti kusini mwa Lebanon kutoka mto Litani hadi mpakani.

    Nchi hizo mbili zitakutana tena tarehe 22 Juni kufanya mazungumzo zaidi "kwa lengo la kufikia makubaliano kamili". Hezbollah bado haijatoa maoni hadharani kuhusu tangazo hilo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio aliwaambia waandishi wa habari kabla ya tangazo hilo kwamba alitumai watatoa "mpango wa utekelezaji katika njia ya usalama huko [Lebanon], bila kutegemea Hezbollah".

    Soma zaidi:

  17. Hujambo na karibu katika matangazo yetu mubashara. Tarehe ni 04/06/2026.