Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Wakazi wakimbia mji wa Lebanon huku Israeli ikionya kufanya mashambulizi

Jeshi la Israel latoa agizo la kuhamishwa kwa mji wa kusini wa Tiro - ikiwa ni pamoja na sehemu ya Wakristo - likisema litachukua hatua "kwa nguvu".

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga

  1. Tetesi za soka Jumanne: Tottenham wanaendelea na mazungumzo ili kumnasa Savinho

    Tottenham wanaendelea na mazungumzo kuhusu dili la takribani £60m kwa ajili ya winga wa Manchester City, Mbrazili Savinho, mwenye umri wa miaka 22. (Mail)

    Manchester United bado wana nia ya kumsajili Elliot Anderson, huku viongozi wa klabu wakiwa na matumaini ya kuipiku Manchester City katika mbio za kumnasa kiungo huyo Muingereza mwenye umri wa miaka 23, anayekadiriwa kuwa na thamani ya takribani £100m na Nottingham Forest. (Guardian)

    Inasemekana Anderson ameonesha nia ya kujiunga na Manchester City badala ya Manchester United. (Talksport)

    Atletico Madrid na FC Barcelona zipo katika nafasi nzuri ya kumsajili beki wa Chelsea Marc Cucurella, 26, ambaye anataka mabadiliko baada ya miaka minne Stamford Bridge. (Marca)

    Newcastle United itamfuatilia kiungo wa Monaco, Lamine Camara, 22, endapo Sandro Tonali au Joe Willock wataondoka St James’ Park msimu huu wa joto. (Telegraph)

    Macho ya skauti wa Manchester United yalimfuatilia mshambuliaji chipukizi wa Inter Milan, Pio Esposito, 20, alipokuwa akiichezea Italia dhidi ya Ugiriki katika mechi ya kirafiki. (Teamtalk)

    Mshambuliaji wa Ufaransa wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani, 27, ambaye alicheza kwa mkopo Tottenham msimu uliopita, anataka kujiunga na Juventus. (Tuttosport)

    Manchester City wanafikiria kumsajili winga wa Real Madrid Rodrygo, 25, na Iliman Ndiaye wa Everton na Senegal, 26. (Mail)

    Beki wa kati Mreno Gonçalo Inácio wa Sporting yuko kwenye orodha ya Liverpool FC kama mbadala wa Ibrahima Konaté anayeondoka. (CaughtOffside)

    Atalanta BC wanafanya mazungumzo na Nottingham Forest kumrudisha beki Nicolò Savona, 23, Serie A. (Goal)

    AC Milan wanatarajiwa kufanya duru ya pili ya mazungumzo na kocha wa zamani wa Crystal Palace Oliver Glasner kuwa meneja mpya. (Calciomercato)

  2. Wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza watekwa nyara na kutishiwa kuondolewa figo zao

    Zaidi ya wahamiaji 300 waliokuwa wakielekea Uingereza msimu uliopita wa kiangazi walitekwa nyara, kuteswa na kutishiwa kuondolewa viungo vyao kwa nguvu, BBC imebaini.

    Wanaume hao vijana, wote kutoka Kurdistan ya Iraq, walikamatwa nchini Libya na kundi la wanamgambo ambao walidai fidia ya dola 5,000 kutoka kwa kila familia ya watu hao, na wakatishia kuwatoa figo ikiwa malipo hayatafanyika haraka.

    Tumezungumza na baadhi ya mateka ambao waliachiliwa baadaye, na pia kuona ushahidi wa picha unaoonesha kuwa upasuaji wa kulazimishwa huenda ulifanyika.

    Waliokuwa mateka walionesha ushahidi wa mateso, na walisema walikuwa wakishikiliwa katika mazingira duni sana, huku karibu watu 180 wakiwa kwenye seli moja.

    Mateka mmoja ameripotiwa kufariki, na bado haijulikani ni wangapi wanaoendelea kushikiliwa.

    Wanamgambo hao walipaswa kuwa wanawaongoza wahamiaji kupitia Libya hadi pwani ya Bahari ya Mediterania. Hata hivyo, mgogoro wa malipo ulizuka kati yao na msafirishaji haramu wa watu wa Kurd wa Iraq, Noah Aaron, ambaye alipanga safari hiyo ya wahamiaji.

    Aaron kwa sasa anatumikia kifungo cha miaka 10 jela nchini Ufaransa kwa makosa tofauti ya utakatishaji fedha na usafirishaji haramu wa watu.

    Maelezo kuhusu utekaji nyara huo yaliibuka wakati wa uchunguzi wa hivi karibuni wa BBC kuhusu msafirishaji mwingine wa watu, Kardo Jaf, ambao ulisababisha kukamatwa kwake mwezi uliopita.

    Inaaminika kuwa wasafirishaji hao wawili walikuwa wakifanya kazi pamoja hapo awali. Wote wawili wanatoka katika mji wa Ranya huko Kurdistan ya Iraq, eneo ambalo limeelezwa kuwa “limejaa mitandao hai ya usafirishaji haramu,” kulingana na ripoti ya taasisi ya utafiti ya Uingereza, Chatham House.

    Mwezi Februari, timu ya uchunguzi ya BBC ilikuwa ikifanya utafiti kuhusu Jaf mjini Ranya, wakati ilipofikiwa na mwanaume mmoja wa eneo hilo aliyesema kuwa mtoto wake alikuwa miongoni mwa vijana waliowekwa mateka.

    Unaweza kusoma;

  3. Trump azomewa alipohudhuria mchezo wa mpira wa kikapu, NBA

    Donald Trump amezomewa wakati wa mechi ya mpira wa kikapu mjini New York, akiwa Rais wa Marekani aliyeko madarakani wa kwanza kuhudhuria Fainali za NBA.

    Vishindo vya kuzomewa vilisikika baada ya mashabiki waliokuwa na tiketi kulazimika kusubiri kwa saa kadhaa kwenye mistari mirefu zaidi nje ya Madison Square Garden kutokana na hatua kali za kiusalama zilizoambatana na uwepo wa rais.

    Trump alihudhuria mechi kati ya New York Knicks na San Antonio Spurs katika mchezo wa tatu wa mfululizo wa fainali za NBA za michezo saba. Knicks walikuwa wameshinda michezo miwili ya kwanza.

    Meya wa New York Zohran Mamdani na kundi la watu maarufu pia walihudhuria mchezo huo.

    Tukio la kuzomea lilizuka Jumatatu jioni wakati kamera ilipomuonesha Trump kwenye skrini kubwa ndani ya uwanja, akiwa anatoa saluti wakati mwimbaji akiimba wimbo wa taifa.

    Rais huyo alihudhuria mchezo huo akiwa na mjukuu wake Kai Trump na mmiliki wa New York Knicks, James Dolan, pamoja na baadhi ya maafisa wa utawala wake wakiwemo Waziri wa Uchukuzi Sean Duffy, Waziri wa Mambo ya Ndani Doug Burgum, mkuu wa EPA Lee Zeldin, na mjumbe maalum Steve Witkoff.

    Rais huyo wa chama cha Republican, ambaye alizaliwa katika eneo la Queens mjini New York City, amekuwa na uhusiano mgumu na mji wake wa asili ambao kwa kiasi kikubwa unaunga mkono chama cha Democratic.

  4. Mwamuzi wa Fifa wa Somalia azuiwa kuingia Marekani

    Omar Artan, ambaye alikuwa anatarajiwa kuwa Msomali wa kwanza kuchezesha mechi katika fainali za Kombe la Dunia, ameondolewa kwenye orodha ya waamuzi baada ya kunyimwa kuingia nchini Marekani.

    Artan, aliyekuwa Mwamuzi Bora wa Wanaume wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kwa mwaka 2025, alizuiwa kuingia nchini Marekani akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Miami na kwa sasa yuko nchini Uturuki.

    Hakuna sababu rasmi iliyotolewa na mamlaka za uhamiaji za Marekani kuhusu kurudishwa kwake, lakini Somalia ni miongoni mwa nchi kadhaa zilizowekwa kwenye orodha ya marufuku ya safari iliyowekwa na utawala wa Rais Donald Trump.

    Baada ya kufanya mazungumzo na mamlaka za Marekani, shirikisho la soka duniani FIFA lilisema Artan hatashiriki kwenye michuano hiyo.

    FIFA ilisema: “Tunaweza kuthibitisha kwamba mwamuzi Omar Abdulkadir Artan hataweza kuhudhuria mafunzo na kuchezesha Kombe la Dunia 2026 baada ya kunyimwa kuingia Marekani.”

    FIFA iliongeza kuwa haijihusishi na taratibu za uhamiaji za nchi mwenyeji, ikiwa ni pamoja na utoaji wa visa, na imearifiwa na mamlaka kwamba hadhi ya Artan haitabadilishwa kwa sasa.

    Kwa mujibu wa utaratibu wa awali wa mashindano ya FIFA, serikali ya nchi mwenyeji ndiyo hatimaye huamua nani anapata visa na nani anaruhusiwa kuingia nchini.

    Mshauri mkuu wa Wizara ya Vijana na Michezo ya Somalia alithibitishia BBC kwamba Artan alinyimwa kuingia licha ya kuwa na nyaraka halali.

    Afisa wa ubalozi wa Somalia mjini Nairobi aliiambia BBC kwamba pasipoti ya kidiplomasia ya Artan ilitolewa mahsusi kurahisisha safari yake baada ya changamoto za awali za visa.

    Shirikisho la Soka la Somalia (SFF) limewasiliana na FIFA likitaka ufafanuzi wa haraka.

    Akizungumza na BBC World Service, Andrew Giuliani, anayesimamia Kikosi Kazi cha Ikulu ya Marekani kuhusu Kombe la Dunia, alisema: “Ingawa siwezi kuingia kwa undani kuhusu taarifa hizo, naweza kukuambia kwamba ilikuwa uamuzi sahihi wa mamlaka za forodha na ulinzi wa mipaka na naunga mkono uamuzi huo.”

    Artan alikuwa miongoni mwa waamuzi 52 waliotangazwa na FIFA kuchezesha fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Canada, Mexico na Marekani kuanzia Juni 11 hadi Julai 19.

    Akiwa mmoja wa waamuzi wa ligi ya taifa ya Somalia, Artan alikua mwamuzi wa FIFA mwaka 2018 na pia amewahi kuchezesha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

    Unaweza kusoma;

  5. Vyombo vya habari vya Israel vyamkosoa Trump kwa kumtaka kujizuia kufanya mashambulizi

    Vyombo vya habari vya Israel vimemkosoa Rais wa Marekani Donald Trump kwa kuitaka Israel kutofanya mashambulizi dhidi ya Iran, huku Israel ikiendelea kushambulia Iran licha ya wito huo.

    Baadhi ya wachambuzi wanaona tofauti hizi za hadharani kuwa sehemu ya mkakati mgumu wa kusimamia mvutano huo.

    Tarehe 7 Juni, Israel ililenga makao makuu ya Hezbollah katika kitongoji cha Beirut, hatua iliyosababisha Iran kurusha makombora dhidi ya Israel na kisha Israel kujibu mashambulizi hayo.

    Gazeti la kiliberali la Haaretz liliripoti kwamba Israel ilishambulia Iran “licha ya ombi la Trump kwa Netanyahu.”

    Ingawa Israel na Iran wameepuka mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya kila mmoja tangu mwanzoni mwa Aprili, Benjamin Netanyahu amekuwa akisisitiza mara kwa mara haja ya kurejea kwenye mzozo, jambo linaloibua swali iwapo makubaliano kati ya Marekani na Iran yanaweza kuzuia kikamilifu mpango wa nyuklia wa Iran na pia kutimiza matarajio ya Israel.

    Barak Ravid, mwandishi wa masuala ya kidiplomasia wa Channel 12, alimnukuu afisa mwandamizi wa Marekani na chanzo cha Israel wakisema kwamba Trump alimwambia Netanyahu katika simu: “Usijibu mashambulizi ya makombora ya Iran na ipe diplomasia siku kadhaa zaidi.”

    Gazeti la Haaretz liliandika kwamba: “Asubuhi ya leo ilibainika wazi kuwa juhudi hizo zimeshindwa na kwamba Israel imeishambulia Iran,” likiongeza kwamba pia kombora la balistiki lilirushwa kutoka Yemen.

    Gazeti la Ma’ariv lilitangaza kwamba Israel ina haki ya kujilinda “kwa nguvu, kwa uthabiti na bila kusita” dhidi ya mashambulizi ya makombora ya Iran, huku likikosoa taarifa kwamba Donald Trump alijaribu kuizuia Israel kujibu mashambulizi hayo. Gazeti hilo liliongeza kuwa Marekani inapaswa kuunga mkono hatua za Israel katika mzozo wa pamoja, badala ya kuzuia hatua hizo.

    Unaweza kusoma;

  6. Trump: Nilimwambia Netanyahu kwamba unaweza kuachwa peke yako kukabiliana na Iran

    Siku moja baada ya Iran na Israel kufanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya kila mmoja, Donald Trump alizungumza na vyombo vya habari kwa kina kuhusu juhudi zake za kujaribu kusitisha mzozo huo.

    Trump alisema kwamba alimuonya Waziri Mkuu wa Israel katika simu siku ya Jumapili kwamba “huenda hivi karibuni akabaki peke yake dhidi ya Iran.”

    Marekani pia ilitangaza jana kwamba “haikuhusika” katika mashambulizi ya Israel ya anga na makombora dhidi ya Iran.

    Baada ya wasiwasi kuongezeka kuhusu uwezekano wa vita vikubwa zaidi vya moja kwa moja katika Mashariki ya Kati, Iran na Israel zilitangaza Jumatatu kwamba zitasitisha operesheni za kijeshi dhidi ya kila mmoja.

    Unaweza kusoma;

  7. Habari za asubuhi, karibu katika taarifa zetu za leo