Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Marco Rubio: Kufunguliwa kwa Hormuz ni hatua ya kwanza kuelekea mazungumzo na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa kufunguliwa kwa mlango bahari Hormuz ni sharti la kwanza kwa mazungumzo na Iran, lakini pekee yake haitoshi kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Tumefika tamati ya taarifa zetu kwa siku ya leo, kwaheri!

  2. Marco Rubio: Kufunguliwa kwa Hormuz ni hatua ya kwanza kuelekea mazungumzo na Iran

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema kuwa kufunguliwa kwa mlango bahari Hormuz ni sharti la kwanza kwa mazungumzo na Iran, lakini pekee yake haitoshi kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.

    Rubio alisema kuwa moja ya masharti muhimu ya kupunguza au kuondoa vikwazo ni Iran kujitolea kushiriki mazungumzo maalumu kuhusu akiba yake ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu.

    Pia alitangaza kuwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yataendelea, lakini akasisitiza kuwa hakuna uhakika kwamba mazungumzo hayo yataleta amani.

    Wakati huo huo, shirika la habari la Fars limeripoti kuwa kubadilishana ujumbe kati ya Iran na Marekani “kumesimama kwa angalau siku chache zijazo.”

    Katika maendeleo mengine, licha ya juhudi za Donald Trump za kuingilia kati, mapigano ya kurushiana makombora na mashambulizi kati ya Israel na Hezbollah katika maeneo ya mpakani yanaendelea.

    Unaweza kusoma;

  3. Mazishi ya Khamenei kufanyika baada ya wiki mbili

    Kwa mujibu wa Naibu Mkuu wa Masuala ya Utamaduni na Jamii wa Manispaa ya Tehran, mazishi ya Ali Khamenei yatafanyika "huenda mwishoni mwa mwezi wa Dhul-Hijjah na mwanzoni mwa mwezi wa Muharram," yaani takribani baada ya wiki mbili.

    Mohammad Amin Tavakolizadeh alisema katika mkutano wa 52 wa Tume ya Kijamii na Kitamaduni ya Miji Mikuu ya Iran kwamba jeshi la nchi hiyo ndiyo itakayoratibu shughuli hiyo, na kwamba siku tatu za "maandamano ya wananchi" zimepangwa kama sehemu ya shughuli za mazishi.

    Bw. Tavakolizadeh alisema kuwa baada ya hafla ya kuaga mwili, sala za mazishi na taratibu nyingine za maziko zitafanyika, na shughuli hizo zitadumu kwa takribani saa 24 katika mji wa Tehran.

    "Tunajiandaa kwa idadi ya watu zaidi ya milioni 15 hadi 20 katika mji mkuu," alisema.

    Kwa mujibu wa Tavakolizadeh, baada ya Tehran, shughuli za mazishi zimethibitishwa kufanyika katika miji ya Qom na Mashhad, huku majimbo mbalimbali nchini yakitoa maombi ya kuwa wenyeji wa shughuli hizo za mazishi.

    Alisema kuwa mahali pa mazishi ya Ayatollah Ali Khamenei patakuwa katika hekalu ya Imam Reza mjini Mashhad, "kwa kuzingatia wosia wake na mapendekezo ya ndugu zake."

    Naibu meya wa Tehran alisema kuwa viongozi na waombolezaji kutoka Pakistan, Afghanistan, India, Bangladesh, Kashmir na maeneo mengine ya ulimwengu wa Kiislamu upande wa mashariki wanatarajiwa kusafiri kwenda Mashhad kuhudhuria shughuli hizo.

    Pia alisema kuwa miji iliyoko katika njia ya msafara wa mazishi itakuwa mwenyeji wa hafla za maombolezo kwa angalau siku moja. Miji hiyo ni pamoja na Qom, Karaj, Saveh, Garmsar na Semnan.

    Unaweza kusoma;

  4. Moto wa shule ya Utumishi: Washukiwa 9 kusalia rumande

    Washukiwa tisa wanaohusishwa na moto uliotokea katika Shule ya wasichana ya Utumishi na kusababisha vifo vya wanafunzi 16 wataendelea tena kusalia rumande wakisubiri hatima yao siku ya Jumatano, Juni 3, Citizen imeripoti.

    Wakifika mbele ya Hakimu Mkuu wa Naivasha, Abdulqadir Ramathan, upande wa mashtaka uliomba kuongezewa muda wa siku 30 wa kuwashikilia washukiwa hao ili kukamilisha uchunguzi.

    Ingawa ombi hilo lilipata uungwaji mkono kutoka kwa mawakili wanaowawakilisha waathiriwa, lilipingwa na mawakili wa washukiwa hao.

    Mawakili wa utetezi walidai kuwa sababu zilizotolewa za kuendelea kuwazuilia washukiwa hazikuwa na uzito wa kutosha.

    Hatua ya mahakama kuhusu ombi hilo inatarajiwa kutolewa Jumatano, Juni 3.

    Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Hakimu Mkuu Abdulqadir Ramathan alisema kuwa mahakama itatoa uamuzi kesho mchana kuhusu iwapo washukiwa wataachiliwa kwa dhamana ya fedha au kama upande wa mashtaka utaruhusiwa kuwaweka rumande kwa siku 30 zaidi ili kukamilisha uchunguzi.

    Haya yanajiri baada ya washukiwa hao kuwaeleza wachunguzi sababu zilizowasukuma kutekeleza kitendo hicho.

    Kwa mujibu wa maelezo yao, walikuwa wakipinga mabadiliko yaliyofanywa kwenye ratiba ya mitihani, uamuzi wa shule kuwatoza ada kwa ajili ya shughuli ya kitamaduni, pamoja na ushawishi kutoka kwa wenzao kufuatia mgomo uliotokea katika shule jirani ya wavulana.

    Washukiwa hao walidai kuwa mpango wa kuchoma bweni hilo ulipangwa saa tatu usiku (9:00 p.m.) na kutekelezwa saa sita usiku (12:00 a.m.), takribani saa tatu baadaye.

    Unaweza kusoma;

  5. Waokoaji wa Ukraine waendelea kutoa miili kutoka kwenye vifusi baada ya mashambulizi ya Urusi kuua watu 18

    Shambulio la makombora na ndege zisizo na rubani la Urusi usiku kucha nchini Ukraine limeua watu wasiopungua 18, wakiwemo watoto wawili, katika kile kinachotajwa kuwa mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya Moscow katika miezi ya hivi karibuni.

    Mvulana wa miaka minane na mwanamke aliyekuwa amenaswa kwenye vifusi vya jengo la makazi ni miongoni mwa watu 12 waliouawa katika mji wa Dnipro, kwa mujibu wa maafisa wa eneo hilo.

    Katika mji mkuu wa Kyiv, watu sita walipoteza maisha.

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alisema kuwa miundombinu ya kiraia na vituo vya nishati vililengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku zaidi ya watu 100 wakijeruhiwa.

    Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema mashambulizi hayo yalikuwa jibu kwa mashambulizi ya awali yaliyofanywa na Ukraine.

    Katika taarifa yake, ilidai kuwa “malengo yote ya shambulio” yalifikiwa.

    Kwa upande wake, serikali ya Kremlin ilisema Jumanne kwamba inaendelea kutekeleza mashambulizi ya “kimfumo” ambayo ilikuwa imeahidi kuyafanya baada ya kuishutumu Kyiv kwa kuhusika na shambulio lililosababisha vifo katika bweni la wanafunzi katika eneo la mashariki mwa Ukraine linalodhibitiwa na Urusi mwishoni mwa Mei.

    Ukraine ilisema kuwa ililenga na kushambulia kikosi cha kijeshi cha Urusi.

    “Mwenendo huu utaendelea,” msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, aliwaambia waandishi wa habari Jumanne, akisisitiza kuwa mashambulizi hayo yalikuwa yakilenga miundombinu ya kijeshi ya Ukraine.

    Awali, Zelensky alikuwa ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa “shambulio kubwa” katika hotuba yake ya video ya usiku wa Jumatatu, na kuwataka wananchi kuzingatia kwa makini tahadhari za mashambulizi ya anga.

    Kwa ufupi: Mashambulizi makubwa ya Urusi dhidi ya Ukraine yamesababisha vifo vya watu 18 na majeruhi zaidi ya 100.

    Urusi inasema mashambulizi hayo ni kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Ukraine, huku Kyiv ikidai kuwa ililenga malengo ya kijeshi ya Urusi.

    Unaweza kusoma;

  6. Rais wa Ghana asema muswada wa sheria dhidi ya LGBTQ+ utapitiwa kabla ya kuidhinishwa rasmi

    Rais wa Ghana, John Mahama, amesema kuwa muswada mpya unaolenga kuhalalisha adhabu kali dhidi ya shughuli za LGBTQ+ utapitia uchunguzi wa kisheria kabla ya kuidhinishwa rasmi.

    Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Uingereza, Mahama alisema kuwa mshauri wake wa sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali watauchunguza muswada huo kwa sababu ulikuwa umeletwa bungeni kama muswada wa wabunge binafsi, si muswada wa serikali.

    Muswada huo, uliopitishwa na Bunge la Ghana siku ya Ijumaa, unapendekeza kifungo cha hadi miaka mitatu kwa mtu anayejitambulisha kama mwenye mahusiano ya jinsi moja na mwenye jinsia mbili (bisexual), mwenye utambulisho wa kijinsia tofauti (transgender). Pia unapendekeza kuwepo kwa “wajibu wa kuripoti” vitendo vinavyopigwa marufuku kwa polisi.

    Mahama alisema:

    “Tutauangalia na kuhakikisha kuwa kila kitu kiko sawa.”

    Aliongeza kuwa ikiwa kutakuwa na matatizo yoyote ya kisheria au kiutaratibu, muswada huo utapelekwa kwa Baraza la Taifa (Council of State), ambalo ni chombo chake cha ushauri.

    Tangu aingie madarakani mwaka jana, Mahama amekuwa akishinikizwa na viongozi wa dini kuimarisha sheria zinazopinga mapenzi ya jinsi moja.

    Kwa sasa, mahusiano ya jinsi moja tayari ni kinyume cha sheria nchini Ghana chini ya sheria zilizoanzishwa wakati wa ukoloni wa Waingereza.

    Katika kikao cha maswali na majibu jijini London siku ya Jumatatu, Mahama pia alisema kulikuwa na mapungufu ya kiutaratibu wakati wa kupitishwa kwa muswada huo, na kwamba Spika wa Bunge anashughulikia suala hilo.

    Hii ni mara ya pili kwa wabunge wa Ghana kuunga mkono sheria ya aina hiyo. Muswada unaofanana ulianzishwa kwa mara ya kwanza bungeni mwezi Agosti 2021 baada ya kituo cha rasilimali za LGBTQ+ kufungwa katika mji mkuu wa Accra.

    Muswada huo umezua mjadala mkubwa ndani na nje ya Ghana, huku makundi ya kutetea haki za binadamu yakieleza wasiwasi kuhusu athari zake kwa haki za msingi na uhuru wa watu wa LGBTQ+.

    Unaweza kusoma;

  7. Visa sita vipya vya ugonjwa wa Ebola vyathibitishwa Uganda

    Wizara ya Afya ya Uganda imethibitisha visa sita vipya vya ugonjwa wa Ebola, na hivyo kufanya jumla ya maambukizi yaliyothibitishwa nchini humo kufikia 15.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye X, wizara hiyo ilisema kuwa visa vipya viligunduliwa miongoni mwa watu waliokuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa awali kuwa na Ebola.

    Uganda ilirekodi kisa chake cha kwanza cha Ebola tarehe 15 Mei baada ya kifo cha raia wa DRC ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali binafsi. Tangu wakati huo, visa vingine vya maambukizi vimeripotiwa, ikiwemo kwa baadhi ya wahudumu wa afya.

    Wizara ya Afya pia imetangaza kuwa kwa sasa inafuatilia watu 668 waliowahi kuwa karibu na wagonjwa waliothibitishwa kuwa na Ebola, kama sehemu ya juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo. Wakati huohuo, wagonjwa wawili wa Ebola wameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kupona kabisa ugonjwa wa virusi vya Ebola.

    Katika maendeleo yanayohusiana na afya ya umma, Uganda inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Kukabiliana na Majanga ya Magonjwa cha Africa Centres for Disease Control and Prevention (Africa CDC).

    Kituo hicho kitafanya kazi kama kitovu cha kikanda cha ufuatiliaji wa magonjwa, uratibu wa kukabiliana na milipuko ya magonjwa, msaada wa maabara, maandalizi ya dharura, utafiti, pamoja na kupeleka wataalamu wa afya wakati wa dharura za afya ya umma na milipuko ya magonjwa.

    Unaweza kusoma;

  8. Tetesi za soka Jumanne: Barca, Real Madrid macho kwa Cucurella

    Mustakabali wa beki wa kushoto wa Chelsea, Marc Cucurella, unaonekana kuwa na mashaka baada ya klabu kadhaa kuwasiliana na wawakilishi wake kuhusu uwezekano wa kuondoka Stamford Bridge.

    Atletico Madrid, Barcelona na Real Madrid zinatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazomhitaji mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania mwenye miaka 27.

    Liverpool wana shauku ya kumsajili mshambuliaji wa RB Leipzig, Yan Diomande, lakini bado hawajafikia makubaliano ya awali kuhusu uhamisho wa kijana huyo wa miaka 19 kutoka Ivory Coast.

    Newcastle United wamemtambua beki wa kulia wa Atalanta, Marco Palestra, mwenye miaka 21, kama lengo kuu la usajili wa majira ya joto. Hata hivyo, wanaweza kukumbana na ushindani kutoka Manchester City, Arsenal na Inter Milan.

    Mmiliki mwenza wa Inter Miami, David Beckham, anataka kumwajiri Pep Guardiola kuwa kocha wa klabu hiyo ya MLS baada ya kuondoka Manchester City, lakini Mhispania huyo anaripotiwa kukataa.

    Kiungo wa Ureno Bernardo Silva anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na Barcelona baada ya kuondoka Manchester City.

    Mchezaji huyo wa miaka 31 anadaiwa kutaka uhamisho huo kutangazwa rasmi kabla ya mwisho wa wiki.

    Mshambuliaji wa England Marcus Rashford huenda akalazimika kurejea mazoezini na Manchester United kabla ya msimu mpya kuanza, baada ya mpango wa kuhamia Barcelona, ambako alikuwa kwa mkopo msimu uliopita, kusuasua.

    Manchester United wanataka kumuuza Rashford ili kuongeza bajeti ya usajili ya kocha mkuu mpya Michael Carrick. Ingawa Arsenal, Chelsea, Newcastle na Tottenham Hotspur wanamfuatili. United hawapendi kumuuzia mpinzani wao wa moja kwa moja katika Ligi Kuu England.

    Nottingham Forest watafanya mazungumzo na kiungo wa Ivory Coast Ibrahim Sangare kuhusu mkataba mpya, huku Manchester United na Besiktas wakionesha nia ya kumsajili.

    Kiungo wa Middlesbrough, Hayden Hackney, mwenye miaka 23, ni mmoja wa malengo ya Manchester United. Michael Carrick anamfahamu vizuri kutokana na kipindi chake cha kazi Middlesbrough.

    Mshambuliaji wa Ivory Coast Evann Guessand anatafakari hatua yake inayofuata baada ya kifungu cha makubaliano ya mkopo wake kutoka Aston Villa kwenda Crystal Palace kilichoruhusu usajili wa kudumu kumalizika muda wake.

    Aston Villa wako tayari kumruhusu beki wa kulia wa Hispania Andres Garcia kuondoka kwa mkopo msimu huu wa joto, huku Valencia na Elche zikiwa miongoni mwa klabu zinazomtaka.

  9. Watu wawili wauawa Kenya kwa maandamano ya kupinga kituo cha Ebola cha Marekani

    Watu wawili walipigwa risasi na kufariki katika mji wa Nanyuki katikati mwa Kenya wakati wa maandamano ya kupinga mipango ya Marekani ya kuanzisha kituo cha kutengwa kwa wagonjwa wa Ebola katika kambi ya kijeshi iliyo karibu, BBC imegundua.

    Mmoja wa waathiriwa alipigwa risasi katika eneo karibu na Kituo cha Anga cha Laikipia ambapo maandamano yalikuwa yakifanyika. Alifariki baada ya kufikishwa hospitalini na marafiki zake katika mji huo. Mwathiriwa mwingine alikuwa tayari amefariki alipopelekwa hospitalini na wanajeshi.

    Mazingira ya vifo vyao hayajabainika wazi, na maafisa hawajatoa maoni yoyote kuhusu suala hilo.

    Siku ya Jumatatu, mamia ya waandamanaji waliandamana katika mitaa ya mji huo, wakizuia barabara na kuchoma matairi, huku polisi wakifyatua gesi ya machozi ili kuwatawanya.

    Mpango wa Marekani wa kuanzisha kituo cha matibabu ya Ebola nchini Kenya umezua wasiwasi wa umma kuhusu hatari za maambukizi ya mpakani.

    Kituo hicho cha kutengwa chenye vitanda 50 kitahudumiwa na madaktari wa Marekani na kinakusudiwa kuwatibu raia wa Marekani walioathiriwa na mlipuko wa sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Kenya haijarekodi maambukizi yoyote ya Ebola hadi sasa.

    Ijumaa iliyopita, Mahakama Kuu ilisema ufunguzi wa kituo hicho unapaswa kusimamishwa baada ya kundi la haki za binadamu kufungua kesi mahakamani ikidai kituo hicho kilikuwa "hatari kubwa na zinazokaribia" kwa afya ya umma.

    Soma zaidi:

  10. Marekani yaonya raia wake dhidi ya kusafiri kwenda Kenya

    Serikali ya Marekani imetoa ushauri wa usafiri kwa raia wake nchini Kenya kufuatia maandamano katika mji wa Nanyuki dhidi ya kuanzishwa kwa kituo cha karantini cha Ebola kwa ajili ya Wamarekani.

    Katika ushauri wa tarehe 1 Juni, 2026, Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi ulitahadharisha kwamba maandamano huko Laikipia yanaweza kuenea hadi miji mingine mikubwa, ikiwa ni pamoja na Nairobi, katika siku zijazo.

    Ubalozi ulibainisha kuwa maandamano nchini Kenya mara nyingi huambatana na uwepo mkubwa wa polisi, jambo ambalo linaweza kusababisha usumbufu barabarani na kuongezeka kwa wasiwasi wa usalama.

    "Ubalozi wa Marekani unafahamu kuhusu maandamano ya Juni 1 katika Mji wa Nanyuki, Kaunti ya Laikipia. Maandamano kama hayo yanaweza kutokea katika Mji wa Nanyuki na maeneo mengine ya mijini, ikiwa ni pamoja na Nairobi, katika siku zijazo," serikali ya Marekani ilionya.

    "Fuatilieni vyombo vya habari vya ndani kwa hali ilivyo barabarani, fungeni milango na madirisha ukiwa ndani ya gari na uwajulishe marafiki na familia kuhusu mahali ulipo na usalama wako," ubalozi uliongeza.

    Utawala wa Rais Donald Trump uliwasihi raia wa Marekani wanaoishi au wanaotembelea Kenya kuendelea kuwa makini, kuepuka mikusanyiko ya watu, na kufuatilia kwa karibu ripoti za vyombo vya habari vya ndani kwa ajili ya taarifa zaidi kuhusu hali ilivyo barabarani kabla ya kusafiri.

    Trump amteua Henry Wooster kuwa balozi wa Marekani nchini Kenya

    Wakati huo huo, Rais Donald Trump amemteua mwanadiplomasia mkongwe Henry Wooster kama balozi mpya wa Marekani nchini Kenya, Ikulu ya White House ilitangaza mnamo Juni 1.

    Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Wooster aliteuliwa kuwa Balozi na Mwakilishi wa Marekani katika Jamhuri ya Kenya, akisubiri kuidhinishwa na Seneti ya Marekani.

    Wooster ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu wa miongo kadhaa katika sera za kigeni na mahusiano ya kimataifa, akiwa ameshika nyadhifa kadhaa za juu ndani ya Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani na misheni za kidiplomasia kote ulimwenguni.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Mwanasiasa wa Afrika Kusini atafuta hifadhi Marekani kwa hofu ya kuteswa

    Kwa SJ Du Venage, mjumbe wa baraza la mkoa wa chama cha mrengo wa kulia katika muungano tawala wa Afrika Kusini, amefanya uamuzi wa kuondoka nchini mwake chini ya mpango wa wakimbizi wa Marekani ulioundwa na Rais Donald Trump akisema anahofia kuteswa.

    Kiongozi wa zamani wa vijana katika Chama cha Conservative cha mrengo wa kulia — ambacho kilipinga mwisho wa ubaguzi wa rangi — alisema alikulia katika mazingira ua kuogopa kitakachowapata Waafrika Kusini wazungu kama yeye ikiwa watapoteza udhibiti wa nchi, na kwamba hofu hiyi ameendelea kuwa nayo licha ya kutokutendewa vibaya kwa njia inayoonekana.

    Du Venage, ambaye sasa ni mjumbe wa baraza la chama cha Freedom Front Plus mwenye umri wa miaka 56 katika jimbo la Western Cape, ni miongoni mwa kundi la Waafrika wanaoomba kujiunga na mpango aliouamuru Trump kuwasaidia wazungu wachache wa Afrika Kusini, ambao anadai wanakabiliwa na mateso ya ubaguzi wa rangi- madai ambayo serikali imekanusha.

  12. WHO yajadili mkakati wa kukabiliana na Ebola na Rais wa DRC

    Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amemaliza ziara yake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa kukutana na Rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi.

    Alimweleza rais juu ya juhudi zinazoendelea za kukabiliana na virusi vya Ebola na kusisitiza tena msaada wa WHO kwa DRC wakati inaendelea kukabiliana na mzozo wa kiafya.

    Mkuu wa WHO pia alitoa wito wa kuhusishwa zaidi kwa jamii katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu, akisisitiza haja ya kuimarisha uwezo wa mifumo ya afya katika maeneo yaliyoathirika.

    Dk. Tedros pia anaripotiwa kushutumu vikwazo vya usafiri na mipaka vilivyowekwa na baadhi ya nchi kama kikwazo dhidi ya Ebola, akisema vinadhoofisha uwazi na ugawanaji data.

    Kufikia Mei 31, mamlaka ya Congo inasema watu 321 walithibitishwa kuwa na Ebola, ikiwa ni pamoja na vifo 48 vilivyorekodiwa.

    Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Mawasiliano, wagonjwa sita walikuwa wamepona huku maambukizi 116 yakishukiwa kuendelea kuchunguzwa.

    Wakati huo huo, Wizara ya Uchukuzi ilitangaza kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege huko Bunia Jumatatu, ikisema masharti ya kuanza tena kwa usafiri wa anga yalitimizwa.

    Hata hivyo, iliagiza kuheshimiwa kwa masharti ya usafi yaliyowekwa dhidi ya Ebola.

    Soma zaidi:

  13. Mapigano yanaendelea licha ya Israel na Hezbollah kukubali kusitisha vita

    Mapigano yameendelea kusini mwa Lebanon licha ya Israel na Hezbollah kukubali mpango wa Marekani wa kutekeleza usitishaji mapigano kwa kiasi.

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema amezungumza na pande zote mbili na "walikubaliana kwamba ufyatuaji risasi utasitishwa na pande zote mbili", baada ya Iran kuonya kwamba vitendo vya kijeshi vya Israeli nchini Lebanon ni tishio kwa usitishaji mapigano wa sasa kati ya Marekani na Iran.

    Lebanon ilisema Hezbollah imekubali mpango wa kusimamisha mashambulizi dhidi ya Israel na Israel isiushambulie mji mkuu wa Lebanon Beirut.

    Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alithibitisha makubaliano hayo, lakini alionya kwamba mashambulizi dhidi ya Beirut yataendelea "ikiwa Hezbollah haitaacha kushambulia miji yetu na raia" - akiongeza kuwa jeshi la Israeli bado litafanya kazi kusini mwa Lebanon.

    Hata hivyo, ghasia zilishuhudiwa usiku kucha.

    Hezbollah ilisema imeanzisha mashambulizi matatu dhidi ya vifaru na wanajeshi wa Israeli karibu na vijiji viwili kaskazini mwa Israeli, ikitumia ndege zisizo na rubani na "makombora ya mizinga".

    Jeshi la Israeli lilisema limenasa makombora mawili yaliyofyatuliwa kutoka Lebanon. Hakuna majeruhi walioripotiwa.

    Shirika la Habari la Kitaifa la Lebanon linaloendeshwa na serikali liliripoti mashambulizi ya Israel katika maeneo kadhaa ya kusini na kusema "mlipuko mkali sana" uliutikisa mji wa Debbine.

    Soma zaidi:

  14. Rais wa Senegal atangaza baraza jipya la mawaziri

    Rais wa Senegal Rais Bassirou Diomaye Faye ametangaza baraza jipya la mawaziri lenye wajumbe 30. Hatua hiyo imekuja wiki moja baada ya kuteuliwa kwa mwanauchumi Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo kuwa Waziri Mkuu.

    Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama cha PASTEF kabla ya tangazo hilo, hakukuwa na mwanachama yeyote wa chama cha Ousmane Sonko ambaye alipaswa kujumuishwa katika baraza hilo jipya la mawaziri.

    "PASTEF inatangaza kwamba haitashiriki katika serikali ijayo. Chama hicho kinataja kuwepo kwa tofauti kubwa kuhusu nafasi na jukumu la walio wengi katika mpangilio wa mamlaka ya utendaj," Taarifa hiyo ilisema.

    Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa PASTEF hatimaye walirejeshwa serikalini, akiwemo Dkt. Alioune Dione, Waziri wa Fedha na Uchumi na Waziri wa Afya Ibrahima Sy.

    Tangazo la serikali hilo la Juni Mosi, linaonekana kuwa mchanganyiko wa mwendelezo na mabadiliko, huku mawaziri kadhaa wakihifadhi nyadhifa zao kutoka serikali ya Sonko na wakati huo huo viongozi wa zamani wenye uzoefu wakirejea katika uongozi.

    Senegal inapitia misukosuko ya kisiasa huku wanasiasa wake wawili maarufu zaidi – Rais Bassirou Diomaye Faye na Spika Ousmane Sonko – wakijihusisha katika mvutano mkubwa wa kisiasa.

    Ousmane Sonko, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, aliondolewa katika wadhifa huo siku kumi zilizopita kisha akachaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Taifa la Senegal.

    Wadhifa wa Sonko, ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Aprili mwaka 2024 hadi Mei 2026 ulichukuliwa na Ahmadou Al Aminou Mohamed Lo, Mwana Uchumi mwenye umri wa miaka 60, aliyekuwa afisa wa Benki ya Afrika Magharibi.

  15. Ruto atetea kituo cha Ebola kilichoombwa na Marekani kujengwa Kenya

    Rais William Ruto ametetea mradi wa ujenzi wa kituo cha Ebola kilichoombwa na Marekani huko Laikipia, akiondoa wasiwasi kuhusu mradi huo na kusisitiza kuwa unalenga kuimarisha utayari wa Kenya kukabiliana na ugonjwa wa Ebola.

    Akiongea wakati wa mahojiano na vyombo vya habari katika sherehe za sikukuu ya Madaraka Juni 1, Rais Ruto alithibitisha kwamba aliidhinisha mrada huo binafsi baada ya ombi kutoka kwa Rais Donald Trump, akiutaja kama sehemu ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

    "Rais Trump alipoomba serikali ya Kenya iwaunge mkono kwa kuwa na kituo cha kukabiliana na Ebola katika kambi ya jeshi la anga ya Laikipia, nilikubali kwa sababu ilikuwa makubaliano na ushirikiano na marafiki ambao wameshirikiana na Kenya," alisema Rais Ruto.

    "Kwa miaka 30, 40, serikali ya Marekani imetuunga mkono. Wametumia rasilimali nyingi nchini Kenya kushirikiana nasi katika VVU, UKIMWI, na magonjwa mengine."

    Alisisitiza kuwa kituo hicho hakina tofauti na vingine 23 vya maandalizi ya Ebola ambavyo tayari vipo kote nchini.

    Rais alisema vituo kama hivyo vipo katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Hospitali ya Polisi jijini Nairobi, Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi huko Eldoret, na Hospitali ya Alupe huko Busia.

    Rais Ruto alisisitiza kwamba Kenya huwachunguza takriban wasafiri 3,000 kila siku katika vituo vyote vya kuingia nchini, na hakuna kisa chochote cha Ebola kilichorekodiwa kufikia sasa.

    Aliongeza kuwa mipaka ya ardhini na angani inasalia kuwa katika tahadhari kubwa, na itifaki za karantini na kutengwa tayari zimewekwa kote nchini.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Awaua wanafamilia sita kabla ya kujiua mwenyewe, polisi wanasema

    Mwanafamilia aliyekuwa na bunduki amewaua watu sita wa familia yake, kisha akajiua, katika shambulizi lililohusisha mfululizo wa ufyatuaji risasi siku ya Jumatatu katika jiji la Muscatine mashariki mwa Iowa, mji ulioko ufukweni mwa mto Mississippi kutoka Illinois, polisi wamesema.

    Uchunguzi wa awali kuhusu vurugu za bunduki ulionyesha kuwa ufyatuaji risasi "ulitokana na mzozo wa ndani," Idara ya Polisi ya Muscatine ilisema katika taarifa, ingawa hakuna kilichotajwa haswa kuhusu kile ambacho huenda kilisababisha umwagaji damu.

    Wanne kati ya waathiriwa walipatikana wakiwa wamepigwa risasi hadi kufa ndani ya makazi kulingsna na maafisa wa polisi wakijibu ripoti za kwanza za milio ya risasi muda mfupi baada ya saa sita mchana kwa saa za eneo.

    Ingawa mshukiwa wa muuaji alikuwa ametoroka eneo la tukio kabla ya maafisa kufika, alitambuliwa haraka kama Ryan Willis McFarland, 52, wa Muscatine, na alikuwa kwenye njia ya mji karibu na daraja la watembea kwa miguu, Mkuu wa Polisi Anthony Kies alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

    Wakati maafisa walipokuwa wakizungumza naye, alijiua, polisi walisema.

    Baada ya taarifa kuibuka zikionyesha kuwa huenda kulikuwa na waathiriwa wengine, polisi walipata miili ya watu wengine wawili ambao McFarland aliaminika kuwapiga risasi - mmoja katika nyumba iliyo karibu na mwingine katika biashara.

    Waathiriwa wote waliaminika kuwa wanafamilia wa mshambuliaji huyo, Kies alisema. Hawakutambuliwa hadharani na inasemekana kuwa takriban wawili kati ya waathiriwa walikuwa watoto.

    Mkuu wa polisi aliwaambia waandishi wa habari kwamba McFarland alikuwa na rekodi ya uhalifu hapo awali lakini alikataa kufafanua.

    Soma zaidi:

  17. Mashambulizi makubwa ya Urusi yaikumba Ukraine usiku kucha

    Watu watano wameuawa na makumi kadhaa kujeruhiwa nchini Ukraine baada ya Urusi kuanzisha shambulio kubwa usiku kucha.

    Watu wanne wameuawa huko Dnipro na 16 wamejeruhiwa. Mtu mmoja pia aliuawa huko Kyiv, huku wengine takriban 20 wakijeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Urusi mapema Jumanne.

    Maelfu ya watu walikimbilia mji wa Kyiv huku moshi mwingi ukipanda kutoka katikati ya jiji. Maonyo ya uvamizi wa anga yalikuwa yamewekwa katika sehemu kubwa ya Ukraine.

    Meya wa Kyiv Vitali Klitschko amewasihi watu kukaa majumbani mwao. Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Jiji la Kyiv, Tymur Tkachenko, alisema: "Adui anashambulia kwa makombora ya balestiki".

    Klitschko alisema majengo mawili marefu ya ghorofa yameathiriwa na kuna hofu kwamba watu wamenaswa chini ya vifusi.

    Huku mashambulizi ya Urusi yakiikumba Kyiv hadi asubuhi na mapema, mlio wa ndege zisizo na rubani ilisikika kati ya milipuko mikubwa zaidi kumi na miwili huku mashambulizi yakiendelea.

    Kukatika kwa meme na matukio ya moto pia kumeripotiwa kote jijini na ukubwa wa uharibifu bado hakujabainika.

    Kituo cha viwanda pia kimeshambuliwa huko Zaporizhzhia.

    Soma zaidi:

  18. Hezbollah yakubali kusitisha mashambulizi dhidi ya Israel - Lebanon

    Lebanon inasema Hezbollah imekubali mpango wa Marekani wa kusimamisha mashambulizi dhidi ya Israel na Israel isiushambulie mji mkuu wa Lebanon Beirut.

    Ubalozi wa Lebanon nchini Marekani ulisema "umepokea uthibitisho wa kukubali kwa Hezbollah pendekezo la Marekani la kukomesha mashambulizi kwa pande zote mbili".

    Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alithibitisha makubaliano hayo, lakini alionya kwamba mashambulizi dhidi ya Beirut yataendelea "ikiwa Hezbollah haitaacha kushambulia miji yetu na raia".

    Taarifa hizo zilikuja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema amezungumza na wawakilishi wa Netanyahu na Hezbollah na "walikubaliana kwamba ufyatuaji risasi wote utakoma", baada ya Iran kuonya kwamba vitendo vya kijeshi vya Israeli nchini Lebanon ni tishio kwa usitishaji mapigano wa sasa kati ya Marekani na Iran.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, ubalozi wa Lebanon ulisema kwamba "chini ya mpango uliopendekezwa, mashambulizi ya Israeli kwenye vitongoji vya kusini mwa Beirut yatakoma badala ya Hezbollah kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israeli". Iliongeza kuwa usitishaji mapigano "utaongezwa ili kujumuisha eneo lote la Lebanon".

    Hata hivyo Netanyahu alisema: "Wakati huo huo, IDF [Vikosi vya Ulinzi vya Israeli] itaendelea kuendesha shughuli zake kusini mwa Lebanon kama ilivyopangwa."

    Baada ya Trump kusema pande zote mbili zimekubaliana kuacha kupigana, mapigano mengine yaliendelea.

    Hezbollah ilisema imeanzisha mashambulizi matatu dhidi ya vifaru na wanajeshi wa Israeli karibu na vijiji viwili kaskazini mwa Israeli, ikitumia ndege zisizo na rubani na "makombora ya mizinga".

    Soma zaidi:

  19. Karibu katika matangazo yetu mubashara ya terehe 02/06/2026.